Habari

Mkapa asilipwe mafao – Kiula

Waziri wa zamani wa Ujenzi wa Serikali ya Awamu ya Pili, Bw. Nalaila Kiula, ameishauri serikali kusitisha mafao na marupurupu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kwa madai kuwa alikiuka maadili ya uongozi kwa kufanya biashara akiwa Ikulu.

Na Joseph Mwendapole

 
Waziri wa zamani wa Ujenzi wa Serikali ya Awamu ya Pili, Bw. Nalaila Kiula, ameishauri serikali kusitisha mafao na marupurupu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kwa madai kuwa alikiuka maadili ya uongozi kwa kufanya biashara akiwa Ikulu.

 

Pia amemtuhumu kiongozi huyo kuwa alichokifanya wakati wa utawala wake, ni uroho wa mali na kwamba hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

 

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ufisadi na rushwa serikalini.

 

Alisema hakuna sababu ya kuendelea kumpa mafao kiongozi ambaye hakuwa mwadilifu na aliyekiuka maadili ya dhamana aliyopewa.

 

Bw. Kiula ambaye alikuwa Waziri wakati wa awamu ya Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema anamwonea huruma Bw. Mkapa kutokana na tuhuma nyingi anazokabiliwa nazo wakati wa uongozi wake.

 

“Hata Ibara ya 17 ya Katiba ya CCM inasema kiongozi atosheke na asiwe na tamaa ya mali,“ alikumbusha Bw. Kiula ambaye alikuwa Mbunge wa Iramba Singida kwa miaka 20.

 

Alisema anashangaa kuona rais huyo anafanya biashara akiwa madarakani wakati analipiwa kila kitu na kupewa huku akihudumiwa na serikali hadi mwisho wa maisha yake.

 

Bw. Kiula ambaye alikuwa Waziri wa Ujenzi kati ya mwaka 1991 hadi 1995, alisema: “(Mkapa) aliingia kwa mbwembwe kuwa hatakuwa na suluhu na rushwa lakini akaishia kuwa mfanyabiashara� Rais ana mafao mengi lakini inashangaza kuona mtu kama Rais anakuwa na tamaa,“ alidai.

 

Bw. Kiula aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna haja kwa Bw. Mkapa kutoa maelezo dhidi ya tuhuma zinazoelekezwa kwake badala ya kusingizia kuwa anapumzika na amestaafu.

 

Waziri huyo wa zamani alisema ana uhakika tuhuma kuwa Rais mstaafu alikopa Dola 500,000 za Marekani ili afanyie biashara ni za kweli.

 

Aidha, alisema inashangaza kuona yeye (Kiula) alipokopa Sh. milioni 12 ikawa nongwa na kufunguliwa mashitaka ya rushwa.

 

“Mimi nilikopa Sh. milioni 12 nikapatwa na msukosuko mkubwa sana lakini huyo aliyekopa dola 500,000 hakuguswa,“ alihoji.

 

Alisema Bw. Mkapa alifanya hivyo kwa kuwa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hakuwepo wakati huo na kwamba angekuwa hai asingethubutu.

 

Akizungumzia kesi ya tuhuma za rushwa dhidi yake, alidai ilipandikizwa kwa chuki binafsi za Rais Mkapa kutokana na umaarufu aliokuwa nao wakati huo.

 

“Wakati Mzee Mwinyi ananiteua kuwa Waziri wa Ujenzi alinisifu sana kuwa ni kijana mchapakazi na mwadilifu na alikuwa akinisifu mara kwa mara sasa naona hapo ikawa nongwa na gere,“ alidai Bw. Kiula ambaye mpaka mwaka 2000 alikuwa Mbunge wa Iramba.

 

Aliongeza kuwa hata Mzee Rashid Kawawa alikuwa akimsifu kwa utendaji wake na kwamba hali hiyo huenda ndiyo ilimfanya achukiwe.

 

Waziri huyo wa zamani pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. George Mlingwa, walikuwa watuhumiwa wa kwanza kufikishwa mahakamani kwa rushwa.

 

Kesi yao ilifuatia ripoti ya kamati ya Jaji Warioba ya kuchunguza na kubainisha mianya ya rushwa iliyotolewa mwaka 1996.

 

Katika kesi hiyo, Bw. Kiula alionekana hana hatia lakini mahakama ilimuona Bw. Mlingwa akiwa na hatia. Mlingwa alikata rufaa.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents