Habari

Mmiliki wa baa Dar asakwa kwa mauaji

POLISI inamsaka mmiliki wa baa ya Kabanga Pub iliyopo Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, Gerald Kabanga na mlinzi wa baa hiyo, Selemani Bakari kwa tuhuma za kumpiga mtu hadi kumuua.


NA WAANDISHI WA UHURU


POLISI inamsaka mmiliki wa baa ya Kabanga Pub iliyopo Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, Gerald Kabanga na mlinzi wa baa hiyo, Selemani Bakari kwa tuhuma za kumpiga mtu hadi kumuua.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Aibula Tanda alisema jana kuwa watuhumiwa walimuua Rajabu Ally na kutupa maiti yake kwenye bonde la Kinyerezi.
Alisema watuhumiwa walimpiga hadi kumuua Ally baada ya kumtuhumu kuwa aliiba chupa za bia na glasi zenye thamani ya sh. 10,000.
Tanda alisema polisi walipata taarifa za kupatikana maiti ya Ally kwenye bonde la Kinyerezi juzi, huku ikiwa imeharibika vibaya.
Kamanda huyo alisema awali mmiliki wa baa hiyo na mlinzi wake, walitoa taarifa polisi juu ya kuwepo kwa kundi la majambazi Kinyerezi.
Polisi walipofuatilia, alisema walibaini kulikuwa na kundi la vijana waliokuwa wamedhamiria kumdhuru Kabanga kutokana na sababu ambazo hazikuweza kufahamika.
Kitendo cha Kabanga na mlinzi wa baa hiyo, kukimbia na kujificha kusikojulikana, kimewafanya polisi kuwatuhumu kuhusika na mauaji ya Ally.
Wakati huohuo, mkazi wa jijini Dar es Salaam, aliyetambuliwa kwa jina moja la Emmanuel (35) amekufa baada ya kuanguka kwenye mti wa mnazi wakati akigema pombe.
Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Aveline Luoga alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 usiku Kimara Baruti, Dar es Salaam.
Luoga alisema mtu huyo alianguka chini na kufariki papo hapo na baadaye maiti ilipelekwa katika hospitali ya Mwananyamala kusubiri ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Katika tukio jingine, watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kupatikana na gunia moja la bangi, kete 20 na puri saba.
Luoga aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Gerald Elevison (20) na Mashaka Silvester (30) wakazi wa Dar es Salaam.
Akielezea tukio hilo, Luoga alisema watuhumiwa walikamatwa juzi, saa 6:30 mchana katika eneo la Kinondoni Shamba na Morocco.
Luoga alisema Silvester alikamatwa na gunia moja la bangi na puri saba wakati Elevison alikamatwa na kete 20 zinazodaiwa kuwa ni dawa za kulevya.



Source: Uhuru

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents