Habari

Mshahara wa dhambi mauti

WATU wawili wamekufa mjini hapa, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kumgonga muuza duka na kupinduka.

Na Francis Godwin, Iringa



WATU wawili wamekufa mjini hapa, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kumgonga muuza duka na kupinduka.


Imeelezwa kuwa dereva wa gari hilo alikuwa akitokea eneo la hoteli ya Ismila mjini hapa, huku njiani akiwa amesababisha ajali na hivyo akiwa katika mwendo mkali akikwepa kukamatwa, gari lilimshinda na kumgonga mfanyabiashara na kupinduka.


Wakielezea undani wa tukio hilo kwa waandishi wa habari hizi aliyefika eneo la tukio hilo jana, Bw. Mashaka Mgumba, ambaye ni mlinzi wa duka la mfanyabiashara huyo na Bw. Falsal Hinju, walisema ajali hiyo ilitokea juzi ya saa 4.45 usiku.


Bw. Mgumba alisema akiwa katika shughuli zake za kuimarisha ulinzi katika eneo hilo la RETCO, barabara ya Uhuru mjini hapa, alishuhudia gari hilo likija kwa mwendo mkali, hali iliyomfanya kukimbia.


Hata hivyo, alisema gari hilo lilimgonga mfanyabiashara huyo, Bw. Charles Bob (28), mkazi wa Lugalo ambaye alikuwa nje ya duka lake katika eneo la RETCO akifunga duka.


Alisema baada ya kumgonga mfanyabiashara huyo, gari hilo lilipamia mti ulipo jirani na kupinduka.


Bw. Hinju alisema baada ya gari hilo kupinduka ndipo waliposogea kumwokoa dereva na mfanyabiashara huyo, lakini wakiwa njiani kumkimbiza katika hospitali ya mkoa kwa matibabu, mfanyabiashara huyo alikufa na dereva akafia hospitali ya mkoa, akiwa mbioni kupewa matibabu.


Bw. Hinju alimtaja dereva wa gari hilo, kuwa ni Bw. Omary Kaniki (22) mkazi wa Lugalo, kuwa mazishi yake yalitarajiwa kufanyika jana.


Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Bw. Mohamed Mbwana, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwa gari hilo namba T 221 ARC Toyota Corolla ni mali ya SEBA International Tanzania Limited na kuwa mbali ya marehemu hao, hakuna mtu mwingine aliyejeruhiwa na chanzo cha ajali bado kinachunguzwa na Polisi.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents