Habari

Mtandao wa ujambazi watikisa tena Jiji la Dar

MTANDAO wa ujambazi unaohusisha wanawake umeibuka Jijini Dar es Salaam na umepora magari saba kwa siku tano tangu Aprili Mosi hadi juzi, imeelezwa.

Regina Kumba


MTANDAO wa ujambazi unaohusisha wanawake umeibuka Jijini Dar es Salaam na umepora magari saba kwa siku tano tangu Aprili Mosi hadi juzi, imeelezwa. Majambazi hao ambao wamejikita kupora magari aina ya Toyota Corolla wamekuwa wakitimiza azma yao kwa kuyakodi na hadi jana hakuna hata gari moja lililokuwa limepatikana.


Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Abdallah Mssika, alisema jana kuwa majambazi hao wamekuwa wakikodi magari hayo ambayo ni teksi na baadaye kuyapora.


Mssika alisema siku ya kwanza, Aprili Mosi saa 6 mchana, Omary Mbwana (43) akiwa na gari T 329 ACZ Toyota Corolla rangi ya damu ya mzee, alikodiwa na watu wawili kutoka Ubungo kwenda Mwenge na njiani walimkaba na kumpora gari hilo.


Alisema siku iliyofuata saa 6.30 mchana, John Denis (27) akiwa na gari namba T 645 AFX Toyota Corolla nyeupe, alikodiwa na mtu mmoja kutoka Kituo cha Reli kwenda ukumbi wa Sigara Chang’ombe na baada ya kufika huko waliingia wote na kununua sigara, lakini Denis aliporudi nje hakulikuta gari.


Aprili 4, saa 3.30 asubuhi, kwa mujibu wa Kamanda Mssika, Rashid Masoud (60) akiwa na gari T 467 APV Toyota Corolla nyeupe alikodiwa na watu wawili kwenda Kiwanda cha Maji Keko na walipofika alivamiwa na kufungwa miguu na mikono, kuzibwa mdomo kwa plasta na kwenda kumtupa Kiwalani, Yombo.


Alisema Aprili 5, saa 7 usiku, Abdalah Alli (22) akiwa na gari namba T 207 AHG , Toyota Corolla alikodiwa na watu watatu mmoja akiwa mwanamke kutoka Tabata Relini kwenda Mwenge kwa Kakobe na wakiwa njiani walimkaba na kumfunga miguu na mikono na kwenda kumtupa Mbezi Juu.


Pia Kamanda Mssika alisema siku hiyo hiyo saa 1.45 jioni, Abdallah Azizi (22) akiwa na gari namba T 282 AFB Toyota Sprinter, alikodiwa na mtu mmoja kwenda Afrika Sana Mwenge kutoka Magomeni na walipofika, watu wengine wawili walijitokeza na kumtishia na kitu kama bastola na kutoweka na gari.


Aprili 11, saa 1.15 jioni, Musa Omari (43) akiwa na gari T251 AQQ Toyota Corolla, nyeupe, alikodiwa na mtu mmoja kutoka Shule ya Benjamin Mkapa Kariakoo, kwenda Mtaa wa Muheza, Kariakoo na kuongezeka mtu mmoja aliyetaka apelekwe kwa Sheikh Yahaya Magomeni. Njiani walimtishia dereva huyo kwa bastola kichwani, wakamfunga na kwenda kumtupa Kipawa.


Siku hiyo hiyo hiyo saa 5 usiku, Ramadhani Mwalimu (60) akiwa na gari namba T 918 AMX , Toyota Corolla ya rangi ya bluu, alikodiwa na watu wawili mmoja akiwa mwanamke kutoka Muhimbili kwenda Mapambano Sinza na walipofika ukuta wa Shule ya Mapambano walimkaba na kumtoa nje ya gari na kutoweka.


Kamanda Mssika aliwataka wafanyabiashara wa teksi na magari mengine ya kukodi kuwa makini wanapokodiwa.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents