Habari

Mufti apuuza njama za kumpindua

SHEIKH Mkuu Mufti, Issa Shaaban Simba amesema kuwa hana wasiwasi na harakati zinazodaiwa kufanywa na baadhi ya Waislam kutaka kumng’oa madarakani kwa kuwa alichaguliwa na Waislam.

Na Michael Uledi, Dodoma

 

SHEIKH Mkuu Mufti, Issa Shaaban Simba amesema kuwa hana wasiwasi na harakati zinazodaiwa kufanywa na baadhi ya Waislam kutaka kumng’oa madarakani kwa kuwa alichaguliwa na Waislam.

 

Mufti Simba aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Mwananchi mjini Dodoma.

 

Alisema bado ana uwezo wa kuliongoza Baraza Kuu la Waislam (BAKWATA) kwa mujibu wa taratibu zilizomweka madarakani.

 

Aliwataka Waislam na Watanzania kuwa watulivu na kuondoa mashaka juu ya uongozi katika chombo hicho.

 

“ Mimi sina wasiwasi kwa sababu Waislam walinichagua na kwa sasa sijapoteza network (mtandao) na ningali na uwezo wa kuwatumikia kikamilifu,” alisema Shekh Mkuu.

 

Aliwataka Waislam wanaotaka kumng’oa kufuata taratibu zilizomuweka madarakani na kubainisha udhaifu wake.

 

“Nawashauri Waislam na Watanzania kuwa watulivu wakizingatia kuwa baraza limeweka milango wazi, likithibitisha kosa kwa kiongozi yeyote awe wa chini au juu ataondolewa kwa kufuata taratibu,” alisema Mufti Simba.

 

Alisema kuwa kama watu wameona amevunja miiko, utaratibu ni kuitisha Tume ya Dini na kueleza matatizo hayo na ikiyaridhia hapo ndipo taratibu za kumwondoa madarakani zinaweza kufanywa vinginevyo ni kutengeneza majungu.

 

Sheikh Mkuu alisema kuwa taratibu za kumpindua zimekuwa zikiibuka na kupotea na amezichukulia kuwa ni propaganda za kiulimwengu.
Gazeti moja la kila wiki la Machi 9, mwaka huu, lilichapisha habari kuwa kuna watu, wakiwamo waliokuwa viongozi wa Bakwata walioondolewa hivi karibuni wanakula njama kumpindua Sheikh Mkuu.

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents