Burudani ya Michezo Live

Nidhamu kwanza urembo utafuata – Miss Shinyanga 2012

Na Joseph Muhozi – Shinyanga

Wakati heka heka za kuwasaka warembo watakaopanda katika jukwaa moja kumtafuta Miss Tanzania 2012 zikiendelea katika kila mkoa, na huku kamati ya Miss Tanzania ikitoa masharti ya nidhamu kwenye mkataba, huko Shinyanga swala la nidhamu sio tu limekua ni swala la kuzungumzika na kushauriana ama kuwekwa kwenye mkataba,bali ni kigezo rasmi kitakachotumika kumpata mrembo atakayeuwakilisha mkoa huo katika kinyang’anyiro cha kumsaka Miss Lake Zone.
Hii inamaanisha kuwa hata kabla hajasaini mkataba wa nidhamu, kila mrembo anatakiwa awe na nidhamu ya kweli na si kwasababu amebanwa na mkataba!
Akizungumza na waandishi wa habari, mwandaaji wa mashindano ya kumsaka Miss Shinyanga 2012, ambaye pia aliwahi kutwaa taji la Miss Temeke, 1996, Bi.Asela Madaka amesema urembo ni kigezo ambacho washiriki wote wanacho lakini tatizo kubwa ni nidhamu ya warembo hao.
Na katika kuhakikisha kuwa wana ‘walk the talk’ walishawaondoa warembo watano (5) kambini kwa sababu za kinidhamu na hivyo kufanya idadi ya warembo waliobaki kambini kuwa 15 tu kati ya 20 walioanza kambi pamoja.
“Nidhamu kwanza urembo utafuata, hatutaki kutengeneza wakina……………’’(alimtaja mmoja kati ya washindi wa miss Tanzania aliyeongoza kwa skendo mara tu baada ya kulivaa taji la miss TZ mwaka fulani. ‘‘Kwa kweli tutakua very strict this time, kuna points za nidhamu zitakazokusanywa na kupewa majaji siku hiyo ya shindano, kwanza kila mshiriki atapendekeza majina matatu ya washiriki wenzake wenye nidhamu, pia tutapata points kutoka kwa watu wa hoteli warembo wanapokaa, na nyingine kutoka kwa matron na zitamuongezea point mshiriki katika mashindano.’’
Mkoa wa shinyanga sio tu umebarikiwa kuwa na madini adimu ya almasi, lakini pia ni moja kati ya mikoa yenye wasichana wenye muonekano mzuri na wenye mvuto wa aina yake, na wengi wakiwa ni wale wenye rangi ya dhahabu. Na mwaka jana (2011) mshiriki kutoka Shinyanga, Trens Mabula alishika nafasi ya pili katika mashindano ya kumsaka Miss Tanzania 2011.
Shindano la kumsaka Miss shinyanga 2012 limeandaliwa na Asela Promotion ya mjini Kahama na litafanyika tarehe 7/7/2012 katika mji wa Kahama ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi yenye thamani ya sh 1,300,000 (kwa ujumla) na mshindi wa pili atapata zawadi zenye thamani ya sh.1, 250,000.
Mshindi wa tatu atapata zawadi yenye thamani ya shilingi 800,000 na kuanzia nafasi ya nne kila mmoja atapewa fedha taslimu shilingi 70,000.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW