Nusra Mbowe ajeruhiwe msibani

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, almanusura kujeruhiwa kwa kurushiwa mawe na wengine wakitaka kumkata kwa mapanga lakini aliokolewa kwa juhudi za ziada…..

mbowe_1.jpg

 

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, almanusura kujeruhiwa kwa kurushiwa mawe na wengine wakitaka kumkata kwa mapanga lakini aliokolewa kwa juhudi za ziada za polisi waliokuwa katika eneo hilo la mazishi ya Mbunge wa Tarime Mheshimiwa Chacha Zakayo Wangwe.

Kabla ya tafrani hiyo kuzuka, ndugu wa marehemu waliigomea Serikali kumzika Mbunge huyo wakisema hadi uchunguzi mpya ufanyike waweze kujiridhisha kuhusu chanzo cha kifo hicho.

Ratiba ya maziko hayo ilikuwa ianze saa 7 mchana, lakini kuanzia saa tatu asubuhi, ukoo wa Wangwe ulikaa chini ya mwenyekiti wake Profesa Samwel Wangwe na kutoa uamuzi wa kutozikwa marehemu hadi daktari wa familia kutoka Dar es Salaam atakapofika na kuufanyia uchunguzi upya.

Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alifika katika msiba huo saa nane mchana akiwa amefuatana na viongozi wengine wa vyama vya siasa ndipo ghafla vijana walipotoa mabango yaliyokuwa yamebeba ujumbe mbalimbali wakipinga kuwa kifo cha Wangwe ni mipango ya Mungu.

“Hatutaki sura ya Mbowe tunataka mbunge wetu,” walisikika wakisema vijana hao ambao walikuwa tayari kutaka kumpiga mwenyekiti huyo wa Chadema, wakidai kuwa chama chake kimehusika katika kifo cha Wangwe,baadaye wengine walitoa mapanga na mikuki, hali iliyowalazimu polisi kumchukua Mbowe na kumwingiza ndani ya nyumba ambako walikuwa wamekaa wabunge wengine 20.

Kuona hivyo vijana wengine walianza kurusha mawe kuwaelekezea viongozi hao. Viongozi hao kuona hivyo walitimua mbio wakihofia maisha yao.

Baadhi ya viongozi waliotimua mbio pamoja na Mbowe ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Salehe Ramadhan Feruzi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, Zitto Kabwe ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Mwenyekiti wa CCM Mkoani Mara, Makongoro Nyerere na Mjumbe wa NEC wa CCM wa mkoa wa Mara, Christopher Gachuma.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents