Habari

Ofisa TRA amfanyia unyama mwanafunzi

MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Horohoro, mkoani Tanga, Gamba Gaya (50), anatuhumiwa kumteka, kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha pili, mwenye umri wa miaka 16 na kisha kumtelekeza.

na Prisca Nsemwa na Dauson Harold

 

MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Horohoro, mkoani Tanga, Gamba Gaya (50), anatuhumiwa kumteka, kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha pili, mwenye umri wa miaka 16 na kisha kumtelekeza.

 

Ofisa huyo, inadaiwa alifanikisha azma yake hiyo baada ya kumlewesha msichana huyo kwa dawa za kulevya na kumfanya apoteze fahamu.

 

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari katika ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), binti huyo ambaye sasa ana ujauzito wa miezi sita, alidai kuwa alitendewa kitendo hicho kati ya Desemba mwaka jana na Januari 8, mwaka huu.

 

Akisimulia mkasa huo, alisema kuwa, alikuwa anasoma katika Shule ya Sekondari Mkwakwani iliyopo jijini Tanga, na mwanamume huyo alijitokeza kama mfadhili mwenye nia ya kumpatia msaada wa kulipia huduma za masomo, kwa vile wazazi wake hawakuwa na uwezo mkubwa wa kugharamia masomo yake na kwamba hali yake ilikuwa ni duni.

 

“Nakumbuka aliniita kwenye baa iliyopo jirani na nyumbani na kutaka kujua undani wa maisha yangu na familia yetu ili anisaidie, akaninunulia soda aina ya Fanta, kumbe alikuwa ameweka dawa za kulevya na baadaye akaniteka,” alisema.

 

Aliongeza kuwa, mara baada ya kunywa soda hiyo, alijisikia kizunguzungu na baadaye kupoteza fahamu na kujikuta yupo sehemu ambayo hakuifahamu.

 

“Nilishtuka usiku na nikajikuta nipo sehemu ambayo siifahamu na si nyumbani, ila nikaziona nguo za yule baba wakati huo alikuwa ameenda kuoga.

 

“Aliporudi nikamuuliza tupo wapi, akaniambia nikae kimya atanipeleka nyumbani… ndipo nilipoamka na kwenda chooni, nikawa najisikia maumivu makali, nilipojichunguza, nikakuta nimebakwa,” alisema msichana huyo.

 

Aidha, alisema kuwa baadaye akamwambia kuwa akaoge ili ampeleke nyumbani na alipomaliza kuoga, waliingia katika gari aina ya Mark II na kuanza safari kuelekea sehemu ambako hakuifahamu.

 

Baada ya saa mbili, walifika katika jengo lililoandikwa VIP, nyumba ya wageni, Horohoro, na akamtambulisha kwa muhudumu wa TRA, aliyemtaja kwa jina la Mwanahamisi.

 

Alisema alishikiliwa ndani ya nyumba hiyo kwa muda wa mwezi mmoja bila ridhaa yake, huku akipatiwa huduma na Mwanahamisi.

 

Katika kipindi hicho, anasema, Gaya alikuwa anakuja mara kwa mara na kumlazimisha kufanya naye mapenzi.

 

“Nilikuwa nikikataa, alikuwa ananipiga makofi… wakati nilipokuwa najisikia homa, hawakuniruhusu kwenda kupata matibabu,” alisema.

 

Kutokana na vitendo alivyofanyiwa, binti huyo, ameiomba sheria kuchukua mkondo wake.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TAMWA, Ananilea Nkya, katika kipindi hicho cha mwezi mmoja, wakati alipokuwa akibakwa na kupigwa, binti huyo hakuweza kuwasiliana na familia yake.

 

Hata hivyo, siku moja alifanikiwa kuchukua fedha kutoka kwenye suruali ya mwanamume huyo kabla ya kutoroka kurudi kwa mama yake, wilayani Same.

 

Baada ya binti huyo kugundulika kuwa ni mjamzito, mama yake alimshauri kuwasiliana na Gaya ambaye hata hivyo alikana na kumtishia maisha iwapo angeendelea kumbughudhi.

 

Katika kutafuta haki, mama wa binti huyo, Shangwe Eliya Msangi, alipeleka malalamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Same, Ibrahim Marwa, ambaye alimwita mtuhumiwa wilayani Same na kuhojiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya, Narcis Missana.

 

Kwa mujibu wa Missana, maelezo ya mwanafunzi na mtuhumiwa huyo yalipelekwa Kituo cha Polisi Tanga (eneo la tukio), kwa upelelezi zaidi. TAMWA ilipowasiliana na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga, Selemani Nyakipande, alikiri kupokea jalada la kesi hiyo na kudai kuwa, hapakuwepo maelezo ya mwanafunzi aliyepewa mimba.

 

Alieleza kuwa, amemjulisha kwa simu mkuu wa upelelezi Same ili kukamilisha maelezo hayo.

 

TAMWA ilipowasiliana tena na Mkuu wa Upelelezi Same kuhusu kukosekana kwa maelezo ya mwanafunzi huyo, alishangaa na kusema yeye binafsi aliyaona na kumtuma mpelelezi wake kuyapeleka kwa dispatch na kukabidhi Kituo cha Polisi Tanga.

 

Hata hivyo, TAMWA iliendelea kufuatilia kesi hiyo kwa kuwasiliana tena na afande Nyakipande ambaye alikiri kwamba hatimaye maelezo ya mwanafunzi huyo yaliyodaiwa kupotea yamepatikana ndani ya jalada hilo hilo.

 

Kabla ya TAMWA kupiga simu kwa Mkuu wa Upelelezi Tanga, ilidaiwa kuwa Gaya kwa kutumia simu namba 0784-818431, alikuwa akimpigia mama wa mwanafunzi huyo, huku akijitambulisha kama polisi na kumwamuru aende Kituo cha Polisi Chumbageni.

 

TAMWA ilifanikiwa kuwasiliana na mtuhumiwa, Gaya, ambaye alikana tuhuma zote, lakini akasema kuwa aliwahi kumpa lifti mwanafunzi huyo.

 

Afande Nyakipande, aliiambia TAMWA kuwa, kesi hiyo itasikilizwa kwenye eneo la tukio, mkoani Tanga, kwa mujibu wa sheria. Kwa hali hiyo, mwanafunzi huyo atalazimika kusafiri kutoka Same hadi Tanga.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents