Pinda: Tanzania kuwa na umeme kutumia mto Rufiji

Waziri Mkuu Mizengo PindaWAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Tanzania inafikiria kuanzisha mradi mkubwa wa umeme kwa kutumia maji ya mto Rufiji, ikiwa ni njia moja ya kukabiliana na uhaba mkubwa wa nishati hiyo nchini

Rufiji 


 


Mwandishi Maalumu, Maputo


 


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Tanzania inafikiria kuanzisha mradi mkubwa wa umeme kwa kutumia maji ya mto Rufiji, ikiwa ni njia moja ya kukabiliana na uhaba mkubwa wa nishati hiyo nchini.

Alikuwa akizungumza na Waziri Mkuu wa Msumbiji, Luisa Diogo alipomtembelea ofisini kwake mjini hapa jana asubuhi mwishoni mwa ziara yake ya siku tatu kuhudhuria mkutano wa maendeleo ya elimu kwa Afrika.

Pinda alisema mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji ni sehemu ya mpango wa kutafuta vyanzo vingine zaidi vya kuzalisha nishati hiyo yenye uhaba mkubwa nchini.

Aliipongeza Msumbiji kwa kujitosheleza kwa umeme kutoka mradi mkubwa wa bwawa la Cabora Basa lililojengwa tangu ukoloni. Linatoa umeme mkubwa kuliko mahitaji ya Msumbiji na mwingine unauzwa kwa nchi jirani.

Pinda pia alisema kukamilika kwa Daraja la Umoja linalojengwa mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kutafungua maeneo mapya ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Alimweleza Waziri Mkuu huyo mwenzake wa Msumbiji kuhusu hali ya kisiasa nchini, jitihada za kuendeleza elimu, mipango ya kuendeleza afya na mapambano dhidi ya Ukimwi na matatizo ya nishati. Alisema hali ya kisiasa imetengemaa, hatua kubwa zimepigwa kupanua elimu ya msingi; sekondari na ya juu.

Waziri Mkuu Pinda alitoa mwaliko kwa Diogo kutembelea Tanzania wakati atakaoona unafaa baada ya kukamilika kwa taratibu rasmi za mwaliko. Diogo alikubali kimsingi mwaliko huo na akasema ana hakika atajifunza mengi kutoka Tanzania.

Alisema pia kwamba ana hakika Daraja la Umoja litaleta miradi mingine mingi ya pamoja kwa manufaa ya watu wa nchi hizi mbili.

Akiwa Maputo, Waziri Mkuu Pinda alihutubia mkutano wa Umoja wa Kuendeleza Elimu katika Afrika (ADEA) na alikutana kwa mazungumzo ya faragha na Rais Armando Guebuza. Waziri Mkuu alitarajiwa kuondoka hapa jana kurejea Dar es Salaam.


Source: Habari Leo


 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents