Habari

Polisi Dar abaka mtoto kituoni

POLISI wa kituo cha Mabatini- Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, anadaiwa kumbaka mtoto wa kike wa miaka 14 kwa kumuahidi kumsaidia kupata dhamana ili asipelekwe mahabusu.

Na Mwandishi Wa Uhuru

 

POLISI wa kituo cha Mabatini- Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, anadaiwa kumbaka mtoto wa kike wa miaka 14 kwa kumuahidi kumsaidia kupata dhamana ili asipelekwe mahabusu.
Hayo yalidaiwa na mtoto huyo juzi, alipofikishwa kusomewa shitaka la wizi wa simu ya mkononi katika Mahakama ya Watoto ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hamisa Kalombola.
Huku akiangua kilio mbele ya hakimu, mtoto huyo aliieleza mahakama kuwa usiku wa kuamkia juzi, askari wa kituo cha Mabatini alimlazimisha kufanya mapenzi na kumbaka kwa madai angemsaidia kupata dhamana na kwamba asingekwenda mahabusu.
Alidai tukio hilo la kubakwa lilimfika usiku wa kuamkia juzi, alipopelekwa kituoni hapo kwa tuhuma za wizi wa simu.
Alisema wakati akiwa rumande kituoni hapo akisubiri kupelekwa mahakamani kusomewa shitaka, askari huyo alimfuata na kumbaka.
Mtoto huyo ambaye jina lake linahifadhiwa aliangua kilio hicho na kutoa malalamiko hayo baada ya kusomewa shitaka na kukosa wadhamini, ambapo mahakama iliamuru apelekwe rumande ya watoto kama hakuna mtu wa kumdhamini.
“Mama sasa mbona mimi napelekwa mahabusu tena, wakati polisi wa kule kituo cha Mabatini nilikolala, alinibaka akaniambia nisiseme atanisaidia kunipa dhamama ili nisirudishwe tena rumande, sasa mbona narudi rumande jamani,” alilalamika mtoto huyo kwa sauti huku akiweka mikono kichwani.
Mtoto huyo alilia kwa zaidi ya dakika 10 na kulalamikia kitendo hicho anachodaiwa kutendewa na polisi na kwamba hata dhamana aliyoahidiwa hakuipata na matokeo yake alirudishwa rumande ya watoto iliyopo Upanga .
Baada ya kusikia madai hayo, Hakimu Hamisa aliuagiza upande wa mashitaka kumpeleka mtoto huyo kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni ili aweze kuchukuliwa maelezo na yafanyiwe uchunguzi na kama kweli askari amehusika na kitendo hicho achukuliwe hatua.
“Sawa nimesikia, mwendesha mashitaka kesho (jana) mpeleke huyu mtoto kwa mpelelezi mkoa wa Kinondoni aandike maelezo yake na kama kweli huyo askari amehusika, basi taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi yake,”alisema Hakimu Hamisa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Jamal Rwambow akizungumza jana juu ya madai hayo, alisema hana taarifa na tukio hilo, lakini kwa kuwa mahakama imeamuru apelekwe mkoani kwake, atalifuatilia.
Aliongeza kuwa kwa kuwa kitendo anachodaiwa kufanyiwa mtoto huyo siyo kizuri, endapo itabainika ni kweli alibakwa na polisi wa kituo hicho, basi hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi ya mhusika.
Mtoto huyo alisomewa shitaka la wizi wa simu na Mwendesha Mashitaka Pamphil Mhollery, ambaye alidai mtoto huyo mkazi wa Sinza, Dar es Salaam, aliiba simu ya mpangaji wao, Salome Tilio.
Mhollery aliendelea kudai kuwa mtoto huyo aliiba simu hiyo aina ya Nokia yenye thamani ya sh. 280, 000 mali ya Salome, Machi mosi, mwaka huu.
Hata hivyo, mtoto huyo alikana shitaka na baada ya kutoa madai ya kubakwa alirudishwa rumande ambapo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

 

Source: Uhuru

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents