Habari

Richmond yachemka

SASA ni dhahiri kuwa, kazi ya Kamati ya Bunge ya Kuchunguza mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC) ni nzito na inayotiwa vidole ili kuharibu matokeo.

na Irene Mark


SASA ni dhahiri kuwa, kazi ya Kamati ya Bunge ya Kuchunguza mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC) ni nzito na inayotiwa vidole ili kuharibu matokeo.


Katika kukabiliana na hali hiyo, kamati hiyo ya Bunge sasa imeamua kuchukua hatua kadhaa ili kuhakikisha ripoti litakayoitoa inakidhi matarajio ya wananchi na kulinda maslahi ya taifa.


Miongoni mwa hatua ambazo zimechukuliwa na kamati hiyo sasa ni kumuomba Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuiongezea muda wa kazi uliokuwa ukimalizika leo, ombi ambalo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe limesharidhiwa na Spika.


Mbali ya hatua hiyo, kamati hiyo ambayo sasa itafanya kazi kwa wiki mbili zaidi hadi Desemba 31, imelazimika kuwaita tena kwa mahojiano ya chini ya kiapo, baadhi ya mashahidi ikiwa ni pamoja na kuwatuma wajumbe wake kadhaa nchini Marekani yaliko makao makuu ya Richmond ili kukusanya taarifa.


Uamuzi huo unakuja siku moja tu baada ya gazeti hili kuripoti kuhusu kuwapo kwa wasiwasi wa baadhi ya mashahidi kutoa ushahidi wa uongo mbele ya Kamati teule ya Bunge, baada ya kupata mafunzo mahususi ya awali (rehearsal), kutoka kwa maofisa wasiojulikana serikalini.


Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ilitajwa katika gazeti hili kuwa maofisa wake kadhaa walihusika kuwaandaa mashahidi kwa lengo lililoonekana kuwa ni kuharibu ushahidi, ilikana kufanya hivyo.


Taarifa ya maandishi ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Vincent Mrisho iliyotolewa jana, pamoja na kukanusha habari ya jana ya gazeti hili, ilikiri kuhusika kwake katika kazi ya kile ilichokielezea kuwa ni kuratibu maofisa wote waliohusika na ambao wangehitajika kutoa ushahidi mbele ya kamati hiyo ya Bunge.


“Kama serikali ilivyoahidi kutoa ushirikiano wake, serikali, kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati na Madini, ilihusika katika kuratibu maofisa wote waliohusika katika mchakato mzima na kuhakikisha kuwa, wale wote wanaohusika na ambao watahitajika mbele ya kamati; kwanza hawasafiri nje ya nchi ili kuhakikisha uwepo wao iwapo watahitajika mbele ya kamati. Pili, kwa kuwa kazi hii ilifanyika miaka miwili iliyopita, wahakikishe kuwa nyaraka zote muhimu kuhusiana na suala hili zinapatikana ili ziweze kutumiwa na kamati endapo zitahitajika ,” ilisema taarifa hiyo ya Mrisho.


Mrisho alisema serikali inaamini kuwa maelekezo yaliyotolewa kwa maofisa hao yalifanyika si kwa nia ya kuharibu, bali kuhakikisha kuwa nyaraka zote muhimu kuhusu suala hili zinapatikana ili ziweze kutumiwa na kamati endapo zitahitajika.


Wakati Ofisi ya Waziri Mkuu ikikanusha tuhuma hizo, taarifa ya maandishi ya kamati hiyo iliyosomwa mbele ya wanahabari na Mwenyekiti wake Dk. Mwakyembe jana ilikiri kuwapo kwa wasiwasi wa mashahidi kutoa taarifa za uongo.


Mwakyembe alisema hali ya shaka ambayo kamati imeipata kutoka kwa mashahidi hao ni moja ya mambo yaliyosababisha wafikie uamuzi wa kuomba muda wa ziada ili kuwahoji tena wale ambao wana wasiwasi nao.


Alisema wajumbe wa kamati yake wanahisi kuwepo kwa udanganyifu katika ushahidi waliokusanya, hali inayowalazimu kuwaita tena baadhi ya mashahidi na kuwahoji kwa lengo la kubaini ukweli.


“Kuhusu hili la mashahidi baada ya uchambuzi tumegundua kuwa, baadhi yao ushahidi wao wa mdomo ulitofautiana na ule wa maandishi.


“Hivyo basi, kwa kuwa Spika ameturuhusu kuongeza muda, kamati italazimika kuwaita tena baadhi ya mashahidi kuthibitisha kauli zao.


“Watakaothibitika kuipa kamati ushahidi wa uongo wakiwa chini ya kiapo kwa sababu wanazozijua wenyewe, kamati itawachukulia hatua za kisheria, chini ya Sheria ya Kinga, Haki na Maadili ya Bunge,” alisema kwa ukali Dk. Mwakyembe.


Alisema kuwa sheria hiyo inatoa hadi adhabu ya kifungo na iwapo hilo litatokea, itakuwa ni funzo kwa maofisa wa serikali na mashirika ya umma waliotoa ushahidi wao kimzaha wakiamini watalindwa.


Pamoja na suala hilo, Dk. Mwakyembe alithibitisha jana kuwa, kamati hiyo imepeleka wajumbe wake wanne nchini Marekani katika miji ya Houston, Washington na Texas, ili kubaini ukweli kuhusu Kampuni ya Richmond.


Mwenyekiti huyo, aliwataja wajumbe hao kuwa ni Makamu wake, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum, Injinia Stella Manyanya na Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii wote kutoka CCM.


Wengine ni Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Mnyaa (CUF) na Katibu wa kamati hiyo, Anselem Mrema. Timu hiyo iliondoka nchini Desemba 10 na wakiwa Marekani watakusanya taarifa mbalimbali za kampuni hiyo ili kupata ukweli na kujiridhisha kuhusu RDC.


Alisema sababu nyingine ya kwenda Marekani ni kubaini ukweli kuhusu uwezo wa kiutendaji wa kampuni hiyo, kama walivyoagizwa kwenye hadidu za rejea walizopewa na Bunge.


“Wajumbe wa kamati na katibu wapo Marekani tangu Desemba 10. Huko watakutana na maofisa wa ubalozi wetuÂ… wataenda jijini Houston, Washington na Texas, kote huko ni kutaka kujiridhisha kwa sababu tunapokea taarifa muhimu kutoka maeneo tofauti,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa wajumbe hao watarejea nchini kesho.


Alisema taarifa za wajumbe hao kutoka Marekani zitaingizwa kwenye rasimu ya taarifa itakayowasilishwa kwa Spika wa Bunge.


Hali hiyo inakuja wakati taifa likionekana dhahiri kupata hasara kutokana na mradi huo wa Richmond uliogharimu sh bilioni 172.9 kuchukua muda mrefu kukamilika kwake.


Aidha, kuundwa kwa kamati hiyo ni matokeo ya kazi iliyofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, iliyowasilisha taarifa yake ya mwaka 2006/07 iliyotaka kuchunguzwa kwa mkataba wa Richmond.


Awali, mkataba huo ulichunguzwa na Takuru (sasa Takukuru) ambayo katika taarifa yake ya Mei mwaka huu, ilitangaza kubaini kuwapo kwa uzembe huku ikitamka bayana kushindwa kuthibitisha tuhuma zozote za rushwa.


Taarifa ya Takuru iliibua maneno ndani na nje ya Bunge, hali iliyosababisha suala hilo kubakia moja ya ajenda zilizoonekana kuipotezea imani serikali na baadhi ya viongozi wake waliohusishwa katika mkataba huo.


Mbali ya wabunge na Spika Sitta, kuahidi kuwa suala hilo lingefanyiwa kazi, Kamati ya Uwekezaji na Biashara iliendelea kulifuatilia jambo hilo kabla na baada ya taarifa ya Takuru.


Baada ya vuta nikuvute ya miezi kadhaa, Novemba 13 mwaka huu, kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo (CCM) iliwasilisha ripoti kuhusu utendaji kazi wa Tanesco, ikijumuisha suala la Richmond.


Pamoja na mambo mengine, kamati ya Shellukindo ilipendekeza kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuichunguza Richmond kutokana na kubaini kuwapo kwa maswali mengi magumu katika mkataba huo.


Takribani maswali yote yaliyobainishwa na Kamati ya Shellukindo, yalihusisha utata wa mazingira ya kufikiwa kwa mkataba huo tata kati ya Tanesco na Richmond.


Aidha, Kamati ya Shellukindo ilionyesha wazi wasiwasi wake kuhusu mchakato uliosababisha kutiwa saini kwa mkataba huo na mazingira yake yaliyohojiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi Serikalini (PPRA).


Suala jingine lililozua utata ni namna Richmond walivyouza mkataba huo wa kuzalisha umeme wa dharura kwa Kampuni ya Dowans, hatua ambayo hata hivyo ilizidisha mlolongo wa kushindwa kuzalisha umeme wa megawati 100.


Kutokana na kuchelewa huko, kamati hiyo ya Shellukindo ilitaka kuundwa kwa kamati ambayo ingechunguza iwapo Dowans waliokuwa wakipaswa kuilipa serikali dola 10,000 kila siku kwa kipindi walichoshindwa kuzalisha umeme walifanya kama mkataba unavyoelekeza.


Sakata hilo la Richmond lilikuja baada ya taifa kukumbwa na ukame mkali uliosababisha vyanzo vya umeme ambavyo ni maji kukauka kwa kipindi kirefu mwaka jana.


Kutokana na hali hiyo, serikali ilichukua hatua za haraka ili kuepusha nchi isikumbwe na janga la kukosa nishati ya umeme kwa kutafuta kampuni za kuzalisha umeme wa dharura.


Shirika la Umeme nchini (Tanesco) liliingia mikataba na wawekezaji binafsi wa nje kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kutumia gesi asilia na dizeli.


Mbali na Richmond, kampuni nyingine iliyoitikia wito wa serikali kwa haraka ni Aggreko, ambayo ilianza uzalishaji wa umeme wa dharura bila kuchelewa, hivyo kusaidia mapema kuondoa kero na wasiwasi mkubwa uliozikumba sekta za viwanda, biashara na utoaji huduma nchini.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents