Habari

Serikali ina mpango huu ili kijana wa kitanzania asifikirie kuajiriwa

Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde amesema, serikali imekuja na mpango wa kuhakikisha kuwa inamfanya kijana wa Kitanzania asifikirie kuajiriwa. Mpango huo ni wa kumsaidia kijana kupata ujuzi ili aweze kujiajiri na kuajiri wengine.

Mheshimiwa Mavunde ameyasema hayo, Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Aida Kenani lililohoji,

Kwa kuwa utaratibu wa serikali unaeleweka kwa kufuata taratibu mbalimbali na wapo vijana ambao wana sifa hizo, elimu, uzoefu na vitu vingine, Je, ni lini serikali itawapa ajira vijana wa Kitanzania ili kujiepusha na masuala kama ya ukabaji, wizi na mambo mengine?

Akijibu swali hilo Mh. Mavunde amesema “Serikali inaendelea kutoa nafasi za ajira kwa vijana kwa nafasi ambazo zimekuwa zikitangazwa, lakini pia kupitia wizara ya kazi tumeendelea kutoa msisitizo wa kuanza kuwabadilishia vijana mtazamo na kuwaaminisha kuwa, sio lazima vijana wote waende kufanya kazi zote za maofisini na hii muheshimiwa Naibu spika inatokana pia na takwimu iliyofanyika 2014 inatuambia kwamba kundi kubwa linaloingia katika soko la ajira kila mwaka ni kubwa zaidi kuliko nafasi za ajira zinazozalishwa.”

“Kama serikali, tumekuja na mipango kadhaa ya kuhakikisha kuwa tunamfanya kijana huyu wa Kitanzania asifikirie tu jinsi ya kwenda kuajiriwa maofisini lakini tumekuja na mipango mbalimbali, moja wapo ikiwa ni kumsaidia kupata ujuzi ili aweze kujiajiri na kuajiri wengine lakini pia kuwafanya vijana wa nchi hii sasa washiriki kwenye kilimo, ufugaji na biashara ikiwa pia ni sehemu ya ajira.”

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents