Habari

Serikali yakiri ilikurupuka kuagiza spidi gavana

HATIMAYE serikali imekiri kuwa vidhibiti mwendo kwenye magari, vimeshindwa kutumiza malengo ya kupunguza ajali barabarani na kwamba ilikurupuka kuagiza vifaa hivyo bila kufanya maandalizi ya utekelezaji.

Na Ramadhan Semtawa


HATIMAYE serikali imekiri kuwa vidhibiti mwendo kwenye magari, vimeshindwa kutumiza malengo ya kupunguza ajali barabarani na kwamba ilikurupuka kuagiza vifaa hivyo bila kufanya maandalizi ya utekelezaji.


Waziri wa Usalama wa Raia, Harith Bakari Mwapachu, alikiri hilo jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu utekelezaji wa mpango wa kufunga vidhibiti mwendo hivyo na kama umeonyesha tija.


Mwapachu alisema kuna matatizo ya kifundi ambayo yalipaswa kuangaliwa kwanza kabla ya kuagiza vifaa hivyo vifungwe kwenye magari.


Alisema maandalizi hayo ni pamoja na ya kiufundi na kuwahusisha wadau wote kwa kutoa elimu ya matumizi ya vifaa hivyo kabla na baada ya kuagizwa.


” Kuna mapungufu, ambayo ni pamoja na ya kiufundi na yanayohusu wadau, hakukuwa na maandalizi ya kutosha kabla ya kuagiza kuwa vidhibiti mwendo vifungwe katika kila gari,” alisema Mwapachu.


Mwapachu alifafanua kwamba, mtu huwezi kuagiza tu kwamba magari yote yafungwe vifaa hivyo bila kuandaa wadau na kuangalia mambo ya kifundi.


“Ulikuwa kama mradi wa mara moja usiokuwa na maandalizi, matokeo yake madereva wanavifungua wakiwa safarini, ” alisema Mwapachu.


Alipoulizwa kama wizara yake inavifaa vya kutosha vya kuweza kukagua vidhibiti mwendo hivyo na kubaini kama kilifunguliwa njiani, alijibu: “Kwanza sina uhakika kama vifaa hivyo vipo nchini, ndiyo maana nikasema pia kuna technical problem (tatizo la kiufundi).”


” Kuna matatizo ya kimejimenti, tunapaswa kukaa pamoja na wadau wote, tuone jinsi gani tutafanikisha hili,” alisisitiza Mwapachu. 


Alisema mpango huo wa kuagiza vifaa umefanyika lakini kuna mambo mengine kama ubovu wa magari yenyewe ambayo yalipaswa kupewa kipaumbele.


Hata hivyo, Mwapachu alisema kwa sasa kuna Tume maalumu ya serikali inayofanyia kazi sheria zote za usalama barabarani ili kuangalia jinsi ya kuziboresha.


Mwapachu alisema tume hiyo ambayo ilianza kazi tangu yeye akiwa Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba, inahusisha wajumbe kutoka Wizara ya Miundombinu, Tume ya Kurekebisha Sheria na Wizara ya Usalama wa Raia.


Alisema miongoni mwa mambo ambayo tayari yamezingatiwa ni utoaji leseni kwa madereva wa mabasi kwamba lazima wapitie Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) na pia umri wa kupewa leseni hiyo.


Mpango wa serikali kuagiza vidhibiti mwendo ambao ulifanyika mwaka 1998 hadi sasa umeshindwa kuonyesha tija kutokana na madereva kuonekana dhahiri kuizidi ujanja serikali kiufundi, ambapo huvilegeza wakiwa njiani na kuvikaza wakiwa karibu kufika kwenye vituo vya askari wa usalama barabarani bila wao kujua.


Utekelezaji wa mpango huo ulikuwa ni agiza la Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu wa Tatu, Frederick Sumaye, kwa ajili ya kupunguza ajali za barabarani, lakini kumekuwa na ajali nyingi ambazo magari yamebainika kuwa katika mwendo wa kasi zaidi ya kilomita 1000 kwa sasa licha ya kutakiwa kutembea kilomita 80 kama vifaa hivyo vingefanyakazi sawasawa.


Miongoni mwa ajali mbaya ni iliyotokea wiki iliyopita iliyohusisha basi la Buffalo ambalo liliuwa watu 22 na 18 kujeruhiwa vibaya.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents