Habari

Serikali yazindua programu ya kikundi mlezi kwa wanawake wajasiliamali

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amezindua programu ya Kikundi Mlezi yenye lengo la kuwawezesha wanawake wajasilimali wasio katika Sekta rasmi kuleana wenyewe katika kuanzisha na kuendeleza mitaji na biashara zao.


Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akikata utepe kuzindua rasmi Programu ya kikundi Mlezi itakayowezesha wanawake kusaidiana na kuleana wenyewe kwa wenyewe katika kuanzisha biashara ili kujikwamua kiuchumi

Dkt. Ndugulile amezindua programu hiyo wakati alipofanya ziara Wilayani Kisarawe mkoani Pwani katika zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujishughulisha katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Dkt.Ndugulile amesema kuwa ili kufanikisha kufikia Tanzania ya viwanda Serikali itaendelea kuwasaidia wajasiliamali wadogo wadogo hasa wanawake katika kuwawezesha kuanzisha vikundi vitakayoanzisha viwanda vidogo vidogo na vya kati.

Ameongeza kuwa lengo la kuzindua Programu ya Kikundi Mlezi ni inalenga kuwawezesha wanawake wasio katika Sekta rasmi kwa kuwashirikisha wanawake wajasilimali waliokomaa katika biashara kuwalea na kuwasaidia wanawake wajasiliamali wanaoanza shughuli hizo.

“Niseme programu hii itasaidia kwa asilimia kubwa kuibua wanawake ambao hawakuwa na uwezo katika kuanzisha biashara zao na kufanya wanawake kujiunga na vikundi kukuza biashara na miradi yao na hatimaye kuanzisha viwanda vidogo na vya kati”alisisitiza Mhe. Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi.Sihaba Nkinga amesema kuwa programu ya Kikundi Mlezi itasaidia kuwainua wanawake na kujitokeza kwa wingi kujishughulisha na shughuli za uzalishaji.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bw. Musa Gama amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Wizara kuhamasisha wanawake kujitokeza na kujiunga na vikundi na kusaidiana katika kuendesha biashara ambazo zitawasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mmoja wa wanawake wajasiliamali Wilayani Kisarawe Bi. Lydia Jacob ameishukuru Serikali kwa kuzindua Mpango huo utakaowawezesha wanawake kuleana na kusaidiana katika kuanzisha na kuinuka katika biashara ambazo zitawasaidia kujikwamua kiuchumi.

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amefanya ziara ya siku moja mkoani Pwani na kuwatembelea wanawake wajasiliamali katika kuhamasisha wanawake kujishughulisha ili kusaidia kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents