Michezo

SportPesa watinga Afrika Kusini Kibabe: Waikwapua Cape Town City kwa miaka minne

Klabu ya Cape Town City inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Afrika Kusini maarufu kama PSL imekuwa klabu ya kwanza kutoka nchini humo kudhaminiwa na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa.

Wachezaji wa Cape Town City ndani ya jezi mpya za klabu hiyo watakazotumia msimu mpya wa SPL zenye nembo ya SportPesa baada ya kusaini dili la miaka minne na kampuni nguli ya michezo ya kubashiri ya SportPesa, leo Ijumaa ya Agosti 11, 2017.

Klabu hiyo ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi wa Afrika Kusini kwa msimu uliopita wa 2016/17 imeingia kwenye makubaliano ya udhamini kwa mkataba wa rekodi wa miaka minne na SportPesa ambao ndio watakuwa wadhamini wao wakuu kwenye jezi zao pamoja na kuwa washirika rasmi wa klabu hiyo katika michezo ya kubashiri.

Mkurugenzi wa SportPesa Afrika Kusini, Nick Ferguson pamoja na Mmiliki wa klabu ya Cape Town, John Comitis wamesaini makubaliano hayo jijini Cape Town leo Ijumaa  Agosti 11 2017 huku magwiji hao wa michezo ya kubashiri duniani wakitambulisha uwepo wao kwenye Ligi hiyo ambayo inatajwa kuwa ligi tajiri zaidi barani Afrika.

Tunawakaribisha washirika wetu wa kwanza nchini Afrika Kusini ambao ni Cape Town City FC kwenye familia yetu ya SportPesa. Udhamini huu ni uthibitisho kutoka SportPesa kuwa tumejidhatiti katika kuhakikisha tunachangia maendeleo ya mpira wa miguu kwenye nchi hii, Tuna furaha kubwa sana kufanya kazi na Cape Town City FC, klabu ambayo inaendana na thamani yetu na tunatazamia kuwa na kipindi cha mafanikio ambacho kitahamasishwa na safari hii ambayo tumeianza pamoja”, amesema Ferguson Mkurugenzi wa SportPesa Afrika Kusini.

Nembo ya SportPesa itakuwa inaonekana upande wa mbele wa jezi rasmi ya klabu ya Cape Town City baada ya timu hiyo kuingia kwenye orodha ya timu kubwa za mpira wa miguu duniani zinazodhaminiwa na kampuni hiyo.

Makubaliano hayo yanahusisha timu ya wakubwa, timu B na timu za vijana za Cape Town City, ambazo zitashiriki kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika mwaka 2018 baada ya kumaliza nyuma ya klabu ya Bidvest Wits na Mamelodi Sundowns kwenye msimamo wa Ligi ya Afrika Kusini.

Klabu hiyo ilianzishwa na mfanyabiashara maarufu nchini humo, John Comitis ambaye ni mmiliki wa zamani wa Cape Town Spurs na mwanzilishi wa Ajax Cape Town mwaka 2016 ambapo ndipo Cape Town City FC ilizaliwa upya ikiwa ni miongoni mwa vilabu vilivyotamba nchini Afrika Kusini katika miaka ya 1960 na 1970.

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents