Habari

Sunflag yapigwa ‘stop’

MAMLAKA ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) imekiamuru Kiwanda cha Nguo za Sunflag kusimamisha mara moja unyunyiziaji dawa katika vyandarua baada ya wafanyakazi sita wa kiwanda hicho kupoteza fahamu.

Paul Sarwatt, Arusha


MAMLAKA ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) imekiamuru Kiwanda cha Nguo za Sunflag kusimamisha mara moja unyunyiziaji dawa katika vyandarua baada ya wafanyakazi sita wa kiwanda hicho kupoteza fahamu.


Wafanyakazi hao walipoteza fahamu na kulazwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru walipokuwa kiwandani hapo wakinyunyiza dawa aina ya ngao katika vyandarua, kama kinga ya ugonjwa wa malaria.


Inadaiwa kuwa wafanyakazi hao walifanya kazi hiyo bila kuwa na vifaa vya kujikinga, hali iliyosababisha baadhi yao kuathiriwa na sumu ya dawa hiyo. Akizungumza na HabariLeo jana, Ofisa Mkaguzi Mwandamizi Johnas Gao alisema uamuzi huo umefikiwa ili kutoa nafasi ya kufanya uchunguzi juu ya suala hilo na kuepusha madhara zaidi kwa wafanyakazi.


“Tayari tumewaandikia barua juzi na wameipokea na leo tumefuatilia zaidi kuhakikisha kama kweli wamesimamisha unyunyiziaji dawa katika kitengo hicho cha vyandarua, ”alieleza.


Alisema idara yake imetumia Sheria ya Usalama kazini namba 5 kifungu 51 ya mwaka 2003 ili kupisha uchunguzi wa kitaalamu kuhusu suala hilo.


Sanjari na kusimamisha unyunyiziaji dawa hiyo, maofisa wa kiwanda hicho na baadhi ya wafanyakazi wamehojiwa kama hatua ya awali ya upelelezi, alisema. “Lakini pia tutawahoji wahanga wa tukio lenyewe kupata ukweli juu ya matumizi ya vifaa vya kujikinga na madhara ya dawa waliyokuwa wakinyunyiza,” alisema Gao.


Habari zaidi zilizopatikana jana kutoka katika kiwanda hicho zilieleza kuwa baadhi ya maofisa wa ngazi za juu walifikia uamuzi wa kunyunyiza dawa hiyo katika vyandarua baada ya kupata soko la haraka la vyandarua kutoka moja ya nchi za Afrika.


Hata hivyo unyunyiziaji huo ulikwenda kinyume na maelekezo ya watengenezaji wa dawa ya ngao kampuni ya PSI, yanayoeleza kuwa dawa inapaswa kuwekwa kwenye vyandarua na mtumiaji.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents