T-Respect yafanya mapinduzi

Mkurugenzi wa bendi ya TOT, maarufu sasa kama T-Respect, Kapteni mstaafu John Komba, amesema kwamba wamefanya mapinduzi ya hali ya juu, hivyo wapinzani wao wakae chonjo kwani wanakuja na ‘spidi’ kali

na Dina Zubeiry




MKURUGENZI wa bendi ya muziki wa dansi ya TOT, maarufu sasa kama T-Respect, Kapteni mstaafu John Komba, amesema kwamba wamefanya mapinduzi ya hali ya juu, hivyo wapinzani wao wakae chonjo kwani wanakuja na ‘spidi’ kali.

Komba alisema hayo jana mjini hapa, wakati bendi hiyo ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama TOT Plus ilipowatambulisha waandishi wa habari nyimbo zake tatu mpya sambamba na wanamuziki wapya mara baada ya kusukwa upya.

Alisema ana uhakika na bendi yake kufanya vizuri hivi sasa kutokana na uongozi thabiti wa meneja wa bendi hiyo, Ali Choki ambaye anajua nini cha kufanya, pia ni mwenye bidii na anaitambua kazi yake ipasavyo.

Utambulisho huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Saadan mjini hapa ambako, wanamuziki walionyakuliwa na bendi hiyo kutoka nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) walitambulishwa.

Nyimbo hizo ni pamoja na ‘Dhamana Lawama’ uliotungwa na Ali Choki na ‘Riziki Zengwe’ ambao umetungwa na Badi Bakule ‘Jogoo la Mjini’, na ‘Intro’ ambako wanatarajiwa kuingia studio wiki hii kwa ajili ya kurekodi albamu yao itakayokuwa na nyimbo saba.

Nyimbo zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu hiyo na watunzi kwenye mabano ni pamoja na ‘Daktari Wangu’ (Badi Bakule), ‘Liwalo na Liwe’ (Abdul Misambano), ‘Willy Simon’ (Choki na Rogart Hegga), ‘Slow Down’ (Choki) na Intro dakika 9 za kucheza.

Safu ya unenguaji na marapa wa bendi hiyo walitoa burudani ambayo imeonyesha mabadiliko, huku pia safu ya uimbaji ikiongozwa na Choki, Bakule, Hega, Rashid Mwezingo, Esther Lazaro, na Jua Kali, Elite Pembele na Greyson Semsekwa wakifunika kwa rap safi.

Mara baada ya utambulisho huo, Choki alisema wataingia studio na kurekodi nyimbo hizo ambazo wataanza kuzipiga kwa mashabiki wao ili wazizoee kabla ya kufanya uzinduzi rasmi wa bendi hiyo ambayo kwa sasa ipo kambini mjini hapa kwa ajili ya maandalizi yao.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents