Tanzania haistahili kuomba chakula nje – Mengi

Bw. MengiTanzania haistahili kuomba chakula nje ya nchi kwani ina ardhi kubwa na yenye rutuba ambayo ikitumika vizuri inaweza kuzalisha chakula kingi na kuuza kingine nje ya nchi


 



Bw. Mengi


 


Na Joseph Mwendapole



 


Tanzania haistahili kuomba chakula nje ya nchi kwani ina ardhi kubwa na yenye rutuba ambayo ikitumika vizuri inaweza kuzalisha chakula kingi na kuuza kingine nje ya nchi.

Hayo yalisemwa jana na Balozi wa Kupambana na Njaa wa WFP Tanzania, Bw. Reginald Mengi, wakati wa kutangaza matembezi ya kuhamasisha watu kuchangia chakula kwenye shule mbalimbali nchini.

Alisema Tanzania imejaliwa ardhi kubwa na yenye rutuba ambayo ikitumika vizuri, inaweza kupata vyakula vingi na hata kuuza nje ya nchi na kutoa msada kwa nchi zenye njaa.

Bw. Mengi alisema uwekezaji kwenye kilimo si wa muda mrefu kama uchimbaji wa madini hivyo wakulima wakinuia kuzalisha kwa wingi wanaweza.

“Enzi za miaka ya 70 wakati wa kilimo cha kufa na kupona, watu walilima sana na vyakula vikapatikana kwa wingi…na sasa tukiamua kuondokana na njaa, tunaweza hata tukazalisha cha ziada na kusaidia wengine,“ alisema.

Aidha, aliongeza kuwa chakula kikipatikana kwa wingi ni dhahiri mahudhurio ya wanafunzi shuleni yataongezeka na watasoma kwa bidii tofauti na sasa ambapo njaa imesababisha wengine kuacha kwenda shuleni.

Alisema hata wazazi watahamasika kuwapeleka watoto wao shule endapo watakuwa na uhakika kuwa watapata chakula.

“Ifikie wakati Tanzania ijitosheleze kwa chakula, hata WFP wakisikia tunajitosheleza kwa chakula, watafurahi sana. Tumebarikiwa ardhi kubwa na yenye rutuba. Sisi si watu wa kukosa chakula, tunapaswa kuzalisha zaidi na kusaidia wengine na sio kuomba,“ alisema.

Alishauri wakulima wapatiwe vivutio vitakavyosababisha wazalishe kwa wingi.

Aliongeza kuwa, asilimia 40 ya chakula kinachozalishwa nchini kinapotea kutokana na kukosekana sehemu bora za kuhifadhia chakula kinachozalishwa.

Alisema inasikitisha kuona maghala yaliyojengwa kwa ajili hiyo hivi sasa yanatumika kama ofisi na matumizi mengine huku vyakula vikikosa sehemu ya kuhifadhiwa.

Kuhusu soko huria, Bw. Mengi alisema kuna haja kwa serikali kuhakikisha inadhibiti bei badala ya kuacha kila mtu akijipangia bei anayotaka.

Alisisitiza wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia chakula shuleni ili kuwavutia wanafunzi kuhudhuria kwa wingi shuleni.

Alisema lengo la matembezi ya Juni Mosi mwaka huu ni kuelimisha umma wa Watanzania kuelewa umuhimu wa kuchangia chakula kwa wanafunzi.

“Lengo letu jamii nzima ijue tatizo lilivyo na iingilie kati kutafuta suluhu kwa kusaidia vyakula,“ alisema na kuwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha jamii kuhusu tatizo hilo.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents