BurudaniHabari

Tanzania ina ziada ya chakula Tani Milioni 2.6, Waziri Mkuu aeleza

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini imeimarika na kufikia tani milioni 15.9 kwa msimu wa kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 sawa na kuwa na ziada ya tani milioni 2.6.

Pia Serikali inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa kuiwezesha Wizara ya Kilimo kuongeza uwezo wa hifadhi ya Taifa ya chakula kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Aprili 21, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula, Kizota mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema mkakati huo utahusisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa nje ya nchi na hivyo kutoa fursa za ajira na kuwaongezea kipato wananchi.

Amesema Serikali imefungua mipaka na inaendelea na jitihada za kutafuta masoko ya nje pamoja na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa kujenga maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo mengine yenye uzalishaji mkubwa wa chakula.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai , Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama.

Wengine ni Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi na Ajira, Anthon Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Balozi Krzysztof Buzalski.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents