Michezo

Tukimbie hata miguu ikifika kisogoni – Waziri Mwakyembe

Timu ya taifa ya mchezo wa riadha imeagwa rasmi leo na kukabidhiwa bendera ya taifa tayari kwaajili ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia yanayo tarajiwa kufanyika jijini London nchini Uingereza Agosti 4 mwaka huu.

 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe

Timu hiyo yenye jumla ya wachezaji nane imekabidhiwa bendera ya taifa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo DrHarrison Mwakyembe.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Mwakyembe amesema wizara yake iko bega kwa bega na wadau wa michezo hapa nchini katika kuhakikisha kuwa sekta hiyo inapiga hatua.

“Kwanza kabisa nimetiwa moyo sana na ari ya vijana waliyonayo na kama mlivyoona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, vijana hawa wamepikwa vizuri na wana ari, moyo na uzalendo mkubwa na kilicho mbele yao ni kitu kimoja tu, kupambana kufa na kupona na kurudi na medali” amesema Waziri Mwakyembe.

Dkt Mwakyembe ameongeza kuwa “Nilipoangalia viwango vya vijana wa timu yetu ya taifa nilipata faraja sana. Kwani vijana wote hawa wanaviwango vya kimataifa na ndiyo sababu wakapata tiketi ya kushiriki michuano hii ya dunia. Hili siyo swala dogo na napenda niwapongeze sana.

 “Tumeshazijua siri za wenzetu kufanikiwa katika riadha, mazoezi ndiyo kilakitu hata uvae irizi ama utumie madawa huwezi kufanikiwa”.

“Unaposhinda medali unapandishiwa bendera na kupigiwa wimbo wa taifa hiyo ni heshima kubwa, vijana wangu tukimbie hata miguu ikifika kisogoni kimbieni”.

Kwa upande wake rais wa chama cha riadha nchini (RT), Anthony Mtaka amesema kuwa mbali na jitihada kubwa zinazofanywa na chama hicho bado zipo changamoto nyingi ambazo zinahitaji nguvu za pamoja ili kuhakikisha kuwa riadha inaendelea mbele. Amesema kuwa kwa kutambua hilo na kwa kutambua umuhimu wa wadau mbalimbali, wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu sana na wadhamini (DStv) na majeshi mbalimbali kama vile JKT na JW ambapo wanariadha wengi wanatoka.

 

Rais wa chama cha riadha nchini (RT), Anthony Mtaka

Wakati Mkurugenzi mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande amesema kuwa kampuni yake ina dhamira endelevu ya kuibua na kuinua vipaji hapa nchini na ndiyo sababu wakaamua kusaidia katika maandalizi ya timu. “Tmefadhili kwa kiasi kikubwa kambi ya timu iliyokuwa Ilboru Arusha na pia kuhakikisha kuwa timu inawasili Dar es salaam na kujiandaa na safari ya London” amesema   Chande

 

Mkurugenzi mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande

Maharage Chande ameongeza kwa kusema kuwa “Tumekuwa tukimdhamini Balozi wetu Alphonce Simbu kwa mwaka mzima sasa. Matokeo ya nguvu zetu tumeyaona. Ametwaa medali ya dhahabu Mumbai Marathon mapema mwaka huu, pia amevunja rekodi yake London Marathon. Sasa ni miongoni mwa  wakimbiaji wa kutegemewa  hapa nchini”.

Mara baada ya kupokea bendera ya taifa mwanariadha, Alphonce Simbu anayeshiriki mbio ndefu za kilomita 42 amesema kuwa wao wamejiandaa kikamilifu na wanajua wanabeba dhamana kubwa kwa watanzania wote, hivyo watahakikisha kuwa wanapambana na kuleta medali nyumbani.

 

Mwanariadha, Alphonce Simbu(kushoto), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe (katikati) na rais wa chama cha riadha nchini (RT), Anthony Mtaka(kulia)

Jumla ya wanariadha wataoshiriki mbio ndefu za kilomita 42 ni, Alphonce Simbu mwenye rekodi ya 2:09.10 aliyo iweka hivi karibuni katika mashindano ya London Marathon, Ezekiel Jafari Ng’imba 2:11.55 aliyoiweka katika mashindano ya Hannover Marathon mwaka 2017,Stephano Huche Gwandu 2:14.18 mashindano ya Tunis Marathon, Sara Ramadhani Mkera 2:33.08 akishinda katika mashindano ya Dusseldorf mwaka 2017 na Magdalena Crispin Shauri 2:33.28 akishinda katika mashindano ya Hamburg Marathon mwaka 2017.

Wakati washiriki watatu waliyosalia watashiriki mbio fupi, Gerald Geay akishiriki mbio za mita 5000,Emanuel Ginki Gisamoda mita 5000 na Failuna Abdi Matanga akishiriki mbio za mita 10,000.

Mashindano hayo ya dunia ya riadha ya natarajiwa kuanza Agosti 4 mwaka huu na yataendelea kwa muda wa siku 10.

By Hamza Fumo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents