Tupo Nawe

Uchambuzi: Nyimbo 15 kali zaidi za Bongo Flava/Hip Hop zilizotoka kuanzia July 1 – August 2, 2013

Kuanzia July 1 hadi August 2, nyimbo nyingi za Bongo Flava zimeachiwa. Fredrick Bundala aka Skywalker anakuja na uchambuzi wa nyimbo 15 bora zaidi kwa kuzingatia ubunifu wa wimbo wenyewe, uzuri wa mashairi, melody, production, zinavyochezwa redioni na namna zinavyosikilizwa na kupakuliwa (downloaded) mtandaoni.

1. Young Killer ft Bright & Ne-mo – Mrs Superstar

Young Killer anazidi kutoa makucha yake. Hii ni ngoma yake ya pili official baada ya Dear Gambe. Imetengenezwa na producer yule yule aliyemtambulisha nchini, Mona Gangster wa Classic Sounds.

Kwenye Mrs Superstar, Young Killer anawataja baadhi ya mastaa wa kike alio na crush nao wakiwemo Wema, Penny, Diva, Irene Uwoya, Maunda Zorro na wengine. Amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kucheza na majina haya kuendana na matukio ya ukweli kwenye uhusiano wao pamoja na wapenzi wao.

Young Killer ambaye hajafikisha hata umri wa miaka 18, anaendelea kuonesha uwezo mkubwa kiuandishi kiasi ambacho hata wasanii wakubwa wameanza kuuhofia uwezo wake. Mrs Superstar ni ngoma kali mno na imepambwa zaidi na chorus kali ya Bright huku Ne-Mo akiongeza harmony tamu.

Tangu uwekwe kwenye akaunti ya Hulkshare ya Bongo5 tarehe 2 August, Mrs Superstar umeshasikilizwa zaidi ya mara 10,410 na kupakuliwa zaidi ya mara 2,939.Kwenye akaunti ya Dj Choka imesikilizwa mara 9,428 na kupakuliwa mara 2,468.

2. Nay wa Mitego – Salam Zao

Ngoma hii imeingizwa Hulkshare August 2 na hadi sasa imeshasikilizwa zaidi ya mara 9,112 na kupakuliwa kwa zaidi ya mara 1,712 wakati kwenye akaunti ya Dj Choka imesikilizwa mara 7,250 na kupakuliwa mara 2,827. Ni wimbo mkali unaomrudisha Nay kule alikotokea. Hizi ndizo nyimbo zake na mashabiki wake wamemzoea hivyo. Kama kawaida haogopi kuwaponda watu mbalimbali kwa mashairi yasiyo na kificho chochote. Salam Zao ni ngoma yenye beat kali na ina kila sifa ya kuhit.

3. Ommy Dimpoz Ft J Martins – Tupogo

Ommy ameamua kuja kiutuuzima zaidi kwenye Tupogo. Wimbo huu umezungumziwa zaidi hapa. Mpaka sasa tangu uwekwe August 1, umeshasikilizwa zaidi ya mara 7,647 na kupakuliwa mara 1,988. Kwenye akaunti ya Hulkshare ya Dj Choka imesikilizwa mara 6,848 na kupakuliwa mara 2,579.

4. Nikki wa Pili ft Joh Makini – Bei ya Mkaa

Nikki wa Pili amemshirikisha kaka yake kwenye wimbo uitwao Bei ya Mkaa. Beat kali ya wimbo huu imefanywa na Nah Reel huku Chizan Brain akimalizia part ya mwisho ya mchakato wa kurekodi na mastering. Ni ngoma kali ambayo ndugu hao wanatambulisha style mpya, Viburi Flow. Tangu iingizwe kwenye akaunti ya Hulkshare ya Dj Choka July 30, ngoma hiyo imesikilizwa mara 10,916 na kupakuliwa mara 3,812.

5. Cassim Mganga – I Love You

Japo wimbo huu haufanyi vizuri sana kwenye mtandao, tangu utoke haiwezi kupita siku bila kuusikia ukichezwa kwenye redio. Hulkshare uliingia tangu July 3 lakini umesikilizwa mara 2,848 tu na kupakuliwa kwa mara 802 pekee. I love You imemrudisha vizuri Cassim kwenye chart na kwakuwa mashabiki wake wengi ni
wasichana, ngoma hii itaendelea kufanya vizuri.

6. Stamina Ft_Darasa & Warda_Mwambie Mwenzio_(Produced by Tiddy Hotter)

Stamina anaendelea kucheza vyema na maneno na awamu hii uandishi wake unasindikizwa na beat kali ya producer wa Mwanza, Tiddy Hotter. Mwambie Mwenzio umeingizwa kwenye akaunti ya Hulkshare ya Bongo5, tarehe 26 July. Hadi sasa umesikilizwa mara 2,833 Kupakuliwa mara 896.

7. Shilole – Nakomaa Na Jiji

Utakubaliana nami kuwa, Nakomaa na Jiji ni miongoni mwa nyimbo 10 mpya zinazochezwa sana kwenye redio. Ni wimbo mzuri wenye tofauti kubwa na nyimbo nyingi za awali za Shilole.
Hata hivyo pamoja na wimbo huu kuwa mkali, mara zote niusikiapo nimekuwa nikihisi nasikiliza wimbo ninaoufahamu miaka miwili iliyopita. Hadi sasa sijapata jibu la wimbo unaofanana na wimbo huu. Tangu uwekwe July 17, wimbo huu umeshasikilizwa mara 2318 na kupakuliwa kwa mara 347.

8. Godzillah_ft Walter Chilambo –Thanks God

Thanks God uliwekwa kwenye Hulkshare ya Bongo5 July 3. Mpaka sasa umesikilizwa mara 1622 pekee na kupakuliwa mara 526. Hatahivyo, Thanks God inafanya vizuri sana kwenye redio. Production nzuri kutokakwa Marco Chali imeifanya Thanks God kuwa moja ya nyimbo za Hip Hip mwaka huu zenye beat kali kabisa.

Nimewahi kueleza hamu ya kuwepo kwa remix ya wimbo huu ambapo rappers wengine kama 10 hivi washirikishwe na Godzilla kunijibu kuwa atalifikiria hilo. Godzilla kabadilika kwa kiasi kikubwa kwenye wimbo huu.

U50 umepungua humu japo Zilla amepita na ladha za hayati Tupac kiaina. Walter amefanya chorus kali sana na nimependa mwishoni walivyomalizia wimbo wao na kusikika kama wanaimbisha mashabiki.

9. TID Ft Maunda Zoro – Gere

Mnyama hajawahi kukosea tangu arudi kwa Kishindo na Kiuno. Awamu hii ameamua kuitafuta sauti adimu ya Maunda Zorro iliyoongeza utamu kwenye wimbo huu uliotayarishwa na producer Mswaki. Tangu uwekwe July 25, hadi sasa Gere umesikilizwa mara 3,323 na kupakuliwa mara 395.

10. Rama Dee Ft Lady Jaydee – Kama Huwezi

Wimbo huu umeingizwa kwenye akaunti ya Bongo5, July 3. Mpaka sasa umesikilizwa kwa kwa mara 3,376 na kupakuliwa mara 920. Kama Huwezi ni wimbo uliomuonesha Rama Dee si tu kama muimbaji mzuri wa RnB bali muimbaji wa aina nyingine ya ladha ya Kiafrika zaidi. Muunganiko wa sauti tamu ya kike ya Lady Jaydee aka Anaconda na ya kiume ya Rama D aka Baba Abigail, umetengeneza wimbo mzuri unaosikilizwa na rika lolote.

11. Peter Msechu feat_Ally Nipishe – Kibudu

Kila wimbo anaoshirikishwa Ally Nipishe lazima ufanye vizuri zaidi hata ya nyimbo zake mwenyewe. Mfano mzuri ni Mapito ya Mwasiti ilivyohit huku single yake ya kwanza, My japo ni nzuri ikijikuta ikiwa muhanga wa kundi la nyimbo zinazoonekana za kawaida.

Peter alichukua uamuzi sahihi kumshirikisha msanii huyu wa THT na sasa Kibudu inaendelea kufanya vizuri redioni. Tangu iwekwe tarehe 1 August, Kibudu imeshasikilizwa mara 1,147 na kupakuliwa mara 394.

12. Sajna ft. Ben Pol & C-Sir Madini – Ningekuwa Single

Ningekuwa Single ni wimbo ulioyatarishwa na producer wa Tetemesha Records, Kidbway. Tangu uwekwe July 10, wimbo huo hadi sasa umesikilizwa mara 4,863 na kupakuliwa mara 1094. Wimbo huu pia unafanya vizuri redioni.

13. Linex ft Sunday – Kimugina

Ukiniuliza kwanini naupenda wimbo huu, ntakuambia ni chorus yake zaidi japo hata verse zake zimesimama pia. Nimependa namna Linex alivyochanganya lugha tatu kwenye wimbo huu. Mstari wa Kiingereza ameupa ujumbe mzito akisema, “And am not strong enough to handle this kind of love.” Kimugina unajitdi kufanya vizuri kwenye digital downloads kwani tangu umewekwa kwenye akaunti ya hulkshare ya Bongo5, August 2, unaonesha umesikilizwa kwa takriban mara 1,263 na kupakulikuwa mara 488.

14. Dj Choka – Latino Nation (produced by Pancho & Hermy B)

Dj Choka bado ameendelea kujitengenezea brand yake na awamu hii hajacheza mbali sana. Katika Latino Nation amewachukua wasanii walio chini ya label moja naye, B’Hits, Gosby, Deddy, Mabeste na Mrap na ambao hakuna ubishi kuwa hawajamuangusha.

Mpaka sasa Latino Nation imesikilizwa mara 2,220 na kupakuliwa mara 440 tangu uwekwe kwenye Hulkshare ya Bongo5 tarehe 15 July.

15. Ney Lee – Nipe Muda (produced by Mswaki)

Mswaki amenisurprise sana kwenye wimbo huu kwakuwa nimemzoea zaidi kwenye nyimbo za electro/dance na Hip Hop. Ni kazi nzuri inayomweka vizuri Ney Lee hasa kwakuwa alijitambulisha vizuri kwenye wimbo wake wa kwanza, Umekwenda. Hadi sasa Nipe Muda ambayo iliingizwa July 24 umesikilizwa mara 701 na kupakuliwa mara 528.

Bonus: Meninah Atick – Shaghala Baghala

Pamoja na kuendelea kulitumikia kundi lake lake la Shosteez, Menina amepewa uhuru wa kuendelea na project zake binafsi. Wimbo wake mpya, Shaghala Baghala umewekwa Hulkshare ya Bongo5 tarehe 29 July na hadi sasa umesikilizwa kwa zaidi ya mara 400 na kupakuliwa mara 180. Ni wimbo mkali na unadhihirisha jinsi mshiriki huyu wa BSS mwaka jana alivyopevuka kisauti.

Bonus: Cindy Rulz ft Chid bway – Utanifanya Nighairi

Cindy ni miongoni mwa wasanii wachache wa kike wa hip hop waliosalia Tanzania. Ni msanii aliyevumbuliwa na Lamar. Wimbo wake mpya, Utanifanya Nighairi uliingia kwenye Hulkshare ya Bongo5 July 27 na hadi sasa umesikilizwa mara 2,551na kupakuliwa mara 394.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW