UDSM Wacharuka Tena

JINAMIZI la migomo ya wanavyuo katika taasisi za umma za elimu ya juu nchini, limeingia katika hatua mpya baada ya baadhi ya wanavyuo kuwajeruhi wenzao kwa mawe na chupa katika harakati za kuwaondoa wengine madarasani.

 


JINAMIZI la migomo ya wanavyuo katika taasisi za umma za elimu ya juu nchini, limeingia katika hatua mpya baada ya baadhi ya wanavyuo kuwajeruhi wenzao kwa mawe na chupa katika harakati za kuwaondoa wengine madarasani.

Tukio hilo lilisababishwa na vurugu kati ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliogoma wakitaka wapewe asilimia 100 ya mikopo inayojumlisha fedha za kujikimu na ada za masomo na baadhi yao ambao walipinga mgomo huo, baada ya waliogoma kuwalazimisha wenzao kutoka madarasani.

Wanafunzi wawili wamelazwa katika zahanati ya chuo ambao ni Makala Simon mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Uhandisi na Teknolojia ambaye amepigwa jiwe na kujeruhiwa shavu la kushoto.

Pia yupo Benedict Edward aliyejeruhiwa kichwani baada ya kupigwa chupa ya soda kichwani, ambaye hali yake ilizidi kuwa mbaya na akapelekwa Hospitali ya Misheni Mikocheni kwa matibabu zaidi.

Mwingine ni Bahati Aron ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza amejeruhiwa mkononi kwa jiwe, alitibiwa na kuruhusiwa.

Katika hatua nyingi mwandishi na mpiga picha wa Mwananchi, Said Powa alijeruhiwa vibaya katika maeneo mbalimbali ya mwili baada ya kupigwa kwa mateke na ngumi na vitu vigumu kufuatia kuwapiga picha wanachuo hao.

Kundi hilo la wanachuo lilimzonga Powa baada ya kuwapiga picha wakati wakifanya harakati zao za kuwaondoa wanafunzi wengine waliokuwa wakiendelea na vipindi madarasani.

Wakati wakifanya hivyo waligundua kuwa walikuwa wakipigwa picha ndipo walipomkamata mwandishi na kutaka kumnyang’anya kamera na waliposhindwa wakamvamia na kumpiga. Shauri tayari lipo kituo cha polisi Chuo Kikuu na lina jalada namba UD/RB/3436/2008.

Mshauri wa wanafunzi wa chuo hicho, Dk Martha Qorro alisema wahusika wa tukio hilo wanatafutwa na watafikishwa katika vyombo husika.

”Mmoja kati ya wanafunzi waliojeruhiwa ametoka damu nyingi sana na anatarajiwa kushonwa sehemu ya kichwani, wahusika wanatafutwa na tutawafikisha katika vyombo husika,”alisema Dk Qorro.

Dk Qorro alisema Bunge la serikali ya wanafunzi lilikataa kupitisha mgomo huo, baada ya wabunge wengi kupinga mgomo.

”Juzi Bunge la wanafunzi lilikaa kujadili mgomo wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma na wabunge 26 waliunga mkono mgomo huo wakati wabunge 37 wakipinga mgomo huo, lakini asubuhi ya leo nilishangaa kuona baadhi ya wanafunzi wakiandamana,”alisema Dk Qorro.

Vilevile Dk Qorro aliwaomba wanafunzi kuacha mgomo na kurudi madarasani ili kuepusha kufungwa kwa chuo, wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuchangia ada amewataka waende ofisini kwake ili ajue jinsi ya kuwasaidia

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents