Habari

Umri wa urais wapingwa

MKAZI wa Ubungo, Kinondoni Dar es Salaam, Bw. Aristides Buberwa, amefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akipinga kipengele cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinachoweka umri wa mgombea urais kuwa miaka 40.

Na Reuben Kagaruki


MKAZI wa Ubungo, Kinondoni Dar es Salaam, Bw. Aristides Buberwa, amefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akipinga kipengele cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinachoweka umri wa mgombea urais kuwa miaka 40.


Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam jana, Bw. Buberwa alisema amefungua kesi hiyo kwa sababu kipengele hiyo kinawanyima haki vijana wanaopenda kugombea kiti cha urais wenye chini ya umri wa miaka 40.


Alisema katika kesi hiyo namba 28 ya mwaka huu, anasaidiwa na Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).


“Nimeona kuna haja ya kuleta mabadiliko kwa kuitazama upya Katiba…Katiba ya Tanzania ina vifungu ambavyo ni sheria kandamizi,” alisema Bw. Buberwa.


Bw. Buberwa alisema wakati Katiba inaweka umri wa kugombea urais kuwa miaka 40, watu wanaruhusiwa kugombea ubunge wakiwa na umri wa miaka 21.


Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, miongoni wa watu wanaoruhusiwa kukaimu kiti cha urais ni pamoja na Waziri Mkuu.
Alifafanua kuwa Waziri Mkuu anapatikana miongoni wa wabunge, hivyo kuna hatari kukaimu kiti hicho akiwa chini ya miaka 40, jambo ambalo ni kinyume na Katiba.


“Haya ni mambo ya kujiuliza haya, je Waziri Mkuu akiteuliwa kabla hajafikisha miaka 40 na baadaye akateuliwa na Rais kukaimu urais mkanganyiko utaondoka vipi bila sisi kwenda mahakamani?,” alihoji Bw. Buberwa.


Alisema anachotaka ni watu wote wapewe haki ya kugombea uongozi bila kufungwa mikono na kipengele cha umri.


Hoja nyingine iliyomsukuma kufungua kesi hiyo ni kupinga Rais kuteua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


Alisema kwa mfumo wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinatawala, Rais ndiye Mwenyekiti wa chama, hivyo kuna wakati anaweza kulazimika kuteua wajumbe wa Tume watakaotekeleza matakwa ya aliyewateua.


Bw. Buberwa alisema anachotaka ni Tume huru ya Uchaguzi. Kwa upande wa fomu za kugombea uongozi alisema haridhishwi na utaratibu wa sasa wa fomu za kugombea urais kutolewa kwa sh. milioni moja na wabunge sh. 500,000.


Alisema utaratibu huo unawanyima watu masikini haki ya kugombea na kuchaguliwa kama wanakubalika kwa wananchi wao.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents