Habari

Vijana CCM wawatangazia ‘vita’ vigogo

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewaonya viongozi wa ngazi za juu wa serikali chama hicho kutojaribu kuingilia Uchaguzi wao Mkuu unaotarajia kufanyika Desemba mwaka huu.

Na Gladness Mboma

 

 

 

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewaonya viongozi wa ngazi za juu wa serikali chama hicho kutojaribu kuingilia Uchaguzi wao Mkuu unaotarajia kufanyika Desemba mwaka huu.

 

Mwenyekiti wa UVCCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ulinzi, Dkt. Emmanuel Nchimbi aliyasema hayo jana, Dar es Salaam wakati akitangaza ratiba ya uchaguzi huo kuanzia ngazi ya mashina hadi Taifa na kuonya kuwa yeyote atakayeingilia, watamuumbua.

 

Dkt. Nchimbi alisema vijana wanatambua watu watakaowachagua, hivyo hawatapenda kuona mtu yeyote asiye sehemu ya umoja huo akijaribu kuleta ushawishi au kumpigia kampeni mtu kwa lengo la kuugawa umoja huo kwa maslahi yake.

 

Alisema katika Kikao cha Baraza Kuu la Vijana kilichofanyika hivi karibuni mjini Dodoma alitaja mambo ambayo ana mashaka nayo katika uchaguzi huo ambayo ni pamoja na rushwa, utaratibu wa kupakana matope na watu wasiokuwa wanachama kupenyeza mamluki katika uchaguzi huo.

 

“Mimi niliwataka wawe makini, vijana kote nchini waepukane na rushwa, watakaojihusisha au kupakana matope, watachukuliwa hatua, hatutaki mtu atunge maneno dhidi ya mwenzake, hatutavumilia kuona uchaguzi ukiingiliwa na viongozi wa serikali, chama au watu wasiokuwa wanachama wa UVCCM.

 

Vijana hawataki kupandikiziwa viongozi wa kuchongwa ‘hawatafagilia’hata kidogo asitoke mtu au kiongozi mstaafu akatoka na mtu mgongoni mwake nasisitiza vijana hawatamchagua,”alisema Dkt. Nchimbi.

 

Alisema siku ya uchaguzi mtu yeyote atakayetoka nje ya utaratibu katika vikao vya uteuzi atawekwa pembeni nakusisitiza kwamba hawatakuwa wapole katika shughuli hiyo.

 

Dkt. Nchimbi alisema ameamua kuwatahadharisha mapema vigogo ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wakitaka kujiingiza katika uchaguzi huo kuacha mara moja ili wasije kuaibika bure siku hiyo.

 

Mwenyekiti huyo alishangaa swali aliloulizwa na mwandishi mmoja wa habari kuhusu kuwepo kwa baadhi ya watu mikoani walioanza kampeni hizo za uchaguzi na kusema kuwa labda wamejichagua, lakini anachotambua ni kwamba mpaka sasa UVCCM haijateua mtu.

 

Akitangaza ratiba ya uchaguzi huo, Dkt. Nchimbi alisema,ngazi ya mashina utaanza Machi 3 hadi Mei 31 mwaka huu,ngazi ya matawi Juni Mosi hadi Julai 30 mwaka huu.

 

Ngazi ya Kata utafanyika Agosti Mosi hadi Agosti 31 mwaka huu, wakati kwa upande wa Tanzania Visiwani, ngazi ya Jimbo utafanyika Juni Mosi hadi Septemba 30 mwaka huu.

 

Kwa upande wa ngazi ya Wilaya utafanyika Juni Mosi hadi Oktoba 25 mwaka huu na ngazi ya Mkoa ni Juni 20 hadi Desemba 9 na ngazi ya Taifa ni Julai 15 hadi Desemba 13 mwaka huu.

 

Dkt. Nchimbi alisema uchaguzi wa Wilaya kura zitapigwa kwa siku moja ambayo ni Oktoba 25 . Mikoa yote kura siku zitapigwa siku moja Desemba 9 na ngazi ya Taifa utafanyika Desemba 13 hadi 14 mwaka huu.

 

Alisema kuwa sababu za kufanya Uchaguzi huo wa Wilaya na Mkoa kwa siku moja na kisha wa Taifa kwa siku mbili, ni kuwaathiri mabingwa wa rushwa wasipate muda wa kutosha wa kufanya kampeni chafu.

 

Dkt. Nchimbi alisema kuwa viongozi watakaochaguliwa ni wale waliozaliwa kuanzia Januari Mosi mwaka 1978 na kwamba mwanachama wa umoja huo anatakiwa kujiunga akiwa na miaka 14.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents