Habari

Wafadhili wataka ufafanuzi wa tuhuma za ufisadi

SAKATA la tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali na wafanyabiasha nchini linaendelea kutimua vumbi baada ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kutaka serikali itoe ufafanuzi wa kina ili kurejesha imani kwa wafadhili na wananchi.

Waandishi Wa Mwananchi


SAKATA la tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali na wafanyabiasha nchini linaendelea kutimua vumbi baada ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kutaka serikali itoe ufafanuzi wa kina ili kurejesha imani kwa wafadhili na wananchi.


Katika mahojiano Maalum na Mwananchi, Mkuu wa Mabalozi wa EU walioko nchini, Maddens Peter, alisema hadi sasa tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya viongozi hazijakanushwa na akaonya kama serikali itaendelea kukaa kimya basi huenda watu na nchi wafadhili wakadhani kuwa tuhuma hizo ni za kweli.


“Tuhuma zinaonekana bado hazijakanushwa. Serikali inatakiwa kueleza vema kazi, sera na hata mafananikio yake. Mawasiliano ni jambo muhimu sana kwa nchi wafadhili, hivyo ndivyo demokrasia na utawala bora inavyotaka,” alisema.


Peter alisema ni kazi ya serikali kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo ili nchi wafadhili ziweze kuwaeleza wananchi wao.


“Nchi wafadhili wanatakiwa kuwaelezea walipakodi wao jinsi fedha zao zinavyotumika katika nchi hii hivyo tunatakiwa kuwa na ripoti sahihi na ya uhakika ili tuendeleze ushirikiano tuliokubaliana,” alisema.


Kuhusiana na ukaguzi unaoendelea Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Peter alisema nchi wafadhili wana wawakilishi nchini Tanzania wangependa kuona uchunguzi wa kina unafanyika na wakaguzi walioteuliwa.


“Serikali iliwaahidi walipakodi kwamba uchunguzi makini utafanyika na sisi tunasema, si kuwa na ripoti ya ukaguzi tu, lakini pia kuona utekelezaji wa mapendekezo ambayo yatatolewa,” alisema.


Kampuni ya Ernest and Young ambayo imepewa kazi hiyo, ilianza kufanya ukaguzi wa mahesabu BoT Septemba 10, mwaka huu na inatarajia kumaliza kazi hiyo baada ya siku 60.


Wakati huo huo; Balozi Msaidizi wa Ujerumani nchini Tanzania, Ingo Herbert, aliishauri serikali ya Tanzania kujibu shutuma zote za rushwa zinazotolewa dhidi ya baadhi ya viongozi wake kwa sababu nchi wafadhili zinafuatilia kwa karibu malumbano yanayoendelea na kwamba zingependa kufahamu ukweli.


Tuhuma zinazotolewa kuhusu ufisadi ni nzito, nasi tungependa serikali ikatoa tamko lake mapema iwezekanavyo kuhusu tuhuma zilizotolewa na vyama vya upinzani dhidi ya baadhi ya viongozi,� alisema.


Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo, jijini Dar es Salaam jana, Herbert alisema ni vizuri serikali ikazingatia misingi ya utawala bora ambayo dhana yake ni uwazi, ukweli na uwajibikaji.


Alisema Ujerumani ni mshiriki mkubwa wa maendeleo ya Tanzania, kwani katika miongo minne iliyopita imetumia kiasi cha Euro bilioni 1.8 kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo hivyo hata walipa kodi wa Ujerumani nao wangependa kufahamu kuwa kodi zao zinatumiwa vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa.


Herbert alikuwa akieleza kuhusu wiki ya Ujerumani iliyoanza jana, ambayo lengo lake ni kuwatambulisha Watanzania kuwa Ujerumani ni miongozi mwa washirika wakubwa wa maendeleo nchini, hivyo Ubalozi wa nchi hiyo umeandaa maonyesho ya shughuli zake inazofanya Tanzania chini ya taasisi zake za maendeleo ambazo ni Partner for the Future Worldwide (Gtz), Hanns Seidel Foundation (Hsf), Konrad Adenauer-Stiftung (Kas), Friedrich Ebert Stiftung (Fes), Deutsche Welle na Germany Capacity Building International (Inwent).


Alisema serikali ya Ujerumani imeshiriki katika sekta tatu muhimu za maendeleo nchini Tanzania ambazo ni huduma za afya, miradi ya maji safi na salama na uimarishaji wa serikali za mitaa.


Alisema miradi yote hiyo inaendeshwa chini ya mpango wa mashirikiano baina ya Ujerumani na Tanzania ambao lengo lake ni kutekeleza sera ya maendeleo ya Ujerumani ambayo ni kusaidia kunyanyua kiwango cha maisha cha watu wa nchi zinazoendelea.


Herbert alisema katika makubaliano ya ushirikiano baina ya Ujerumani na Tanzania, kipaumbele zaidi kimewekwa katika mpango wa serikali ya Tanzania wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini (Mkukuta), ili kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia ambapo nchi hiyo inaisaidia katika nyanja tatu ambazo ni kukuza uchumi na kupunguza umasikini wa kipato, kuboresha kiwango cha maisha ya watu na huduma za jamii na kukuza utawala bora na uwajibikaji.


Kuhusu suala la utawala bora na uwajibikaji, Herbert alisema wanafuatilia kwa karibu siasa za Tanzania na Ujerumani imeguswa na malumbano yanayoendelea ambayo yanawahusisha viongozi wa serikali ya na tuhuma za rushwa.


Huyu ni balozi wa tatu wa nchi wahisani wa Tanzania kutoa maoni yake kuhusu tuhuma za rushwa na ufisadi zilizotolewa na Dk Wilbroad Slaa dhidi ya viongozi mbalimbali zinazohusisha ufujaji na upotevu wa rasilimali za umma.


Mwishoni mwa wiki iliyopita, Balozi wa Uholanzi Karel van Kesteren, alielezea kukerwa kwake na tuhuma hizo dhidi ya viongozi waandamizi wa serikali na kutaka serikali itoe tamko lake haraka iwezekanavyo.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents