Habari

Wala Rushwa Kupigwa Chini – CCM

Ikiwa ni siku kadhhaa tu tangu kuripotiwa kwa matukio ya rushwa katika mchakato mzima wa kuwapata wagombea wa viti vya ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi ( CCM), chama hicho kimetoa tamko kwa kusema kuwa mgombea yeyote atakayekamatwa na Takukuru kwa kutoa au kupokea rushwa basi hatapitishwa hata kama atashinda katika kura za maoni.

Chama cha mapinduzi kimepongeza mpango mzima wa Takukuru wa kuwanasa wagombea wote wanaojihusisha na rushwa na kusema chama hicho kinaandaa adhabu kali kwa watakaobainika kuhusika moja kwa moja na vitendo vya rushwa.

Mzee Yusuf Makamba ambaye ndio katibu mkuu wa CCM amesema chama kitawafutia matokeo wagombea wote watakaobainika kujihusisha na rushwa katika mchakato huo bila kujali majina na nyadhifa zao ndani ya chama.

Makamba amewaomba wananchi na wanachama wa CCM kukisaidia chama kuwafichua wagombea wote watoa na wala rushwa.

“Wanachama pia watusaidie kwanza kwa kwa kuwafichua na kutowachagua wagombea wa aina hiyo. Na kama ikitokea kwa bahati mbaya wamepita katika kura za maoni CCM haitawapitisha na huo ndio msimamo wetu CCM kwani hatuwezi kumtetea mgombea yoyote anayetoa rushwa,” alisema Makamba.

Kwa upande mwingine Katibu mkuu huyo aliipongeza Takukuru kwa kazi nzito ya kupambana na rushwa na kuitaka iongeze kasi ya kuwafuatilia na kuwachukulia hatua kali pasipo mwogopa mtu.

“Kwa kweli mimi sijapata taarifa rasmi kama kuna wagombea wamekamatwa na Takukuru kwa rushwa, lakini pia napenda kuipongeza Takukuru kwa kazi hiyo nzito na nzuri,na pia iongeze bidii na wana CCM pia washirikiane na Takukuru kufichua watoa na wala rushwa,” alisisitiza Makamba.

Kauli hiyo ya mheshimiwa Makamba imekuja huku taarifa za rushwa zikiendelea kuripotiwa katika kampeni hizo za kura za maoni zilizoanza hivi karibuni.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amewaonya wanasiasa kutojiingiza katika matendo ya rushwa kwa kuwa taasisi yake imejidhatiti kupambana nao na wala haitanii katika suala hilo.

“Takukuru hatutanii, sisi tupo kazini na hatufanyi danganya toto hapa…. hivyo nawasihi wagombea wote wasitoe wala kupokea rushwa,” alisema Dk Hoseah.

Pia alisema mpaka sasa Takukuru imeshakusanya taarifa nyingi tu kuhusu matukio ya rushwa na muda sio mrefu watuhumiwa wataanza kuhojiwa na ikibidi kufikishwa mahakamani.

“Tumeshakusanya taarifa za kutosha hivyo nawasihi wanasiasa pamoja na wananchi kwa ujumla tusilaumiane maana tumejipanga vizuri sana na muda sio mrefu tutaanza kuwahoji na mwisho wa siku tutawakisha mahakamani,” alisema Dk Hoseah.

Kwa mujibu wa takukuru imeeleza kuwa mikoani ndiko kunakoongoza kwa kuwa na wagombea wengi walio kamatwa kwa kutoa rushwa. Akiiainisha mikoa hiyo Dk. Hosea aliitaja kuwa ni Mwanza na Kililmanjaro ambapo Mwanza amekamatwa Mbunge wa Magu,Dk Festos Lumbi akitoa tsh. 500 akimpa mmoja wa wanachama huku Kilimanjaro kuna wanachama watano wa CCM wametiwa mbaroni katika wilaya ya Moshi Mjini kwa kujihusisha na rushwa na kati yao yupo diwani mmoja wa chama hicho japo mpaka sasa bado haijaelezwa walikuwa wakimpigia mbunge gani kampeni.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents