Habari

Wanaowapa mimba wanafunzi wahasiwe – Wabunge

Baadhi wa wabunge, wameiomba serikali kuwahasi wanaume wanaowapachika mimba wanafunzi ili kukomesha vitendo hivyo vilivyoendelea kushamiri nchini.

Na Mary Edward, PST Dodoma



Baadhi wa wabunge, wameiomba serikali kuwahasi wanaume wanaowapachika mimba wanafunzi ili kukomesha vitendo hivyo vilivyoendelea kushamiri nchini.


MBUNGE wa Lulindi, Bw. Suleiman Kumchaya (CCM), aliongea kwa uchungu Bungeni kutokana na mjukuu wake wa darasa la tano kupachikwa mimba.


Alisema kwa vile maagizo mbali mbali ya serikali ya kuwachukulia hatua kali yanashindwa kutekelezeka kutokana na sheria iliyopo kutokidhi haja, njia ya kukomesha vitendo hivyo ni kuwahasi wanaume hao.


“Mheshimwa Naibu Spika, mimi nikiwa ni mmoja wa waathirika wa vitendo hivyo, kutokana na mjukuu wangu wa darasa la tano kupachikwa mimba, nina uchungu sana na hasira na wanaume hao wanaofanya vitendo vya kinyama kiasi hicho,“ alisema.


Alisema watu hao hawatakiwi katika jamii, hivyo suala la kuwahasi itakuwa ni njia pekee ya kuwakomesha watu wenye vitendo kama hivyo.


“Naiomba wizara kama sheria zilizopo hazikidhi, tungeni na mzilete hapa bungeni tuzipitishe�upya ili ziweze kuwaadibisha hao wanaume wenye uchu wa kinyama, maana wanatuharibia watoto wetu.“


Mbunge wa Kiteto, Bw, Kiroya Losurutia (CCM) alisema, serikali haina budi kubadili mtazamo juu ya watu wanaowapa mimba wanafunzi, na badala yake iwahasi ili vitendo hivyo viweze kuisha katika jamii.


“Mheshimwa Naibu Spika, mimi na nafikiri dawa pekee ya kukomesha vitendo hivyo, ni kuwahasi watu hao kwa maana wanarudisha nyuma maendeleo ya watoto wa kike na wazazi wao,“ alisema.


Wabunge wengine waliojadili mjadala huo ni pamoja na Jenister Mhagama Mbunge wa Peramiho (CCM), alisema maagizo mbali mbali yanayotolewa na serikali katika kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaowapa mimba wanafunzi, yamekuwa kama wimbo wa taifa, na watu kuyadharau.


Alisema vitendo hivyo vya mimba vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku, hatua ambayo inaendelea kuwarudisha nyuma wanafunzi wa kike kwa kukosa elimu.


Bi. Susan Lyimo, Viti maalumu (CUF) alisema, wanafunzi wengi wanapewa mimba na wanaume wenye uwezo, wengi wao ni viongozi, wanasiasa wakiwemo madiwani na baadaye kuwatelekeza.


Alisema ili kupunguza vitendi hivyo ni kuwapa uelewa wanafunzi juu ya kuitunza miili yao. Alisema kuna haja ya serikali kupeleka somo la afya ya jamii, ili wanafunzi waelewe umuhimu wa kujitunza baada ya kuingia katika mabadiliko ya utu uzima.


Alisema elimu hiyo itawafanya wafahamu mambo mengi juu ya kujikinga na kujiingiza katika mapenzi wakiwa shuleni na hivyo wengi wa watoto wa kike wataweza kumaliza masomo bila tatizo lolote.


Dk. James Mnanka Wanyancha, Serengeti (CCM) aliishauri serikali kufanya jitihada za kuongeza idadi ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita na kwenda chuo kikuu.


Alisema nguvu nyingi zimeelekezwa katika ujenzi wa shule za msingi na sekondari hadi kidato cha nne, lakini kidato cha tano hadi sita kuna chule chache mno.


Alisema pamoja na mambo mengine, bado idadi kubwa ya wanafunzi wanafeli mtihani wa kidato cha nne na sita na kuitaka serikali kufanya utafiti kuhusu sababu za wanafunzi kufeli sana mitihani hiyo.


Bi. Pindi Chana,�Viti maalumu�(CCM) Iringa alisema serikali iweke mkazo katika kuhakikisha kuwa watoto hawatumikishwi mashambani, katika migodi na majumbani ili wapelekwe shuleni kupata elimu.


Bi. Lediana Mng`ong`o, Viti maalumu� Iringa (CCM) alitaka walimu wanaowapa adhabu kali wanafunzi na kuwasababishia ulemavu, serikali iwachukulie hatua kali za kisheria ili kukomesha hali hiyo.


Kadhalika wale wanaopata mimba waruhusiwe kuendelea na masomo ili waweze kupata elimu itakayowafanya waishi vizuri na watoto wao.


Bw. Kabuzi Faustine Rwilomba, Busanda (CCM) aliiomba serikali iboreshe hali ya elimu mkoani Shinyanga kwa madai kuwa ukosefu wa elimu ndio unaosababisha mauaji ya vikongwe kuendelea.


Mbunge wa Kongwa, Bw, Job Ndugai (CCM) alisema hakuna hata kiongozi wa ngazi ya katibu tarafa kutoka katika wilaya ya Kongwa kutokana na wananchi wake kutokuwa na mwamko wa elimu.


Naye Bi. Nuru Awadhi Bafadhil, Viti Maalumu (CUF) aliishauri serikali kurudisha utaratibu wa (Mobile Clinic) ambao ulikuwa ukitumika zamani ili kupima afya za wanafunzi mara kwa mara na hiyo itasaidia wengi wao kupata mimba wakihofia watagunduliwa shuleni.


Bw. Bujiku Sakila, Kwimba (CCM)� alisema pawepo na chombo maalumu cha kushughulikia matatizo ya walimu kwa vile Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,�amekuwa na mzigo mkubwa hasa kutokana na ongezeko la shule za sekondari nchini.


Bi. Diana Chilolo, Viti maalumu Singida (CCM) alisema serikali iwalipe walimu madeni yao na kuboresha mazingira yao ya kazi ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi zaidi na hatimaye kukuza kiwango cha elimu nchini.


Hivi karibuni mbunge wa Ziwani (CUF) Ali Saidi Salum alishauri wale wanaowapa mimba wanafunzi wanyongwe hadharani na kisha maiti zao ziwekwe kwenye kioo maalum na kuandikwa: “Hawa ni wahalifu wabaya sana.“


Mbunge huyo alishangaa watu wazima kuamua kizini na watoto wa shule badala ya kuwasaidia, wakati kila mahala siku hizi kuna watu wazima waliokubuhu kwa shughuli hiyo.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents