Burudani

Wasanii wa Tanzania kutotoa album ni uzembe, uoga na kutojiamini!

Wasanii wa Tanzania wana sababu nyingi sana za kwanini hawatoi album. Baadhi ya sababu kama kufa kwa mfumo wa uuzaji wa album uliokuwa ukifanywa na wahindi enzi za kanda za redio cassette na urudufuaji usio halali wa kazi zao unaofanywa na wafanyabiashara, zinaweza kueleweka kiasi na kutupa sababu za kuwasamehe.

crimsonking

Lakini imefika wakati sasa wa kuacha kuendelea kuzijengea hofu sababu hizi. Mimi nahisi zimepitwa na wakati na ni muda sasa wa kuthubutu na kufanya mabadiliko. Kwanini tuendelee kuwa na kiwanda cha muziki kisichokuwa na album?

Nilikuwa nikiangalia mahojiano ya hivi karibuni kati ya Clouds TV na Nikki Mbishi kwenye kipindi cha Siz Kitaa na rapper huyo alidai kuwa ukiwa unahojiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, utaulizwa umeshawahi kutoa album ngapi? Hilo ni swali ambalo siku za mbeleni litawaumbua wasanii wengi wa Tanzania. Watakosa jibu la kutoa zaidi ya kujiumauma tu na kamwe sababu hizo mbili ambazo wamekuwa wakizitoa zitaonekana hazina kichwa wala miguu. Lazima iwepo njia mbadala.

Uharamia wa kazi za wasanii wa muziki hauwezi kuisha. Marekani wamejaa wezi kibao, lakini hiyo haijawazuia wasanii wao kuacha kutoa album. Album bado ni kitu muhimu sana kwenye industry. Kwa kupitia album ndipo tunaujua ukweli kama msanii huyu mwenye mashabiki wengi anaweza kweli au anabahatisha tu kwa single moja moja!

Kupitia album, msanii hutengeneza hadithi ya kimuziki ambayo huwa tamu kusikilizwa na shabiki wake. Album ni kipimo cha ukomavu wa msanii, achilia mbali kama itauza ama haitouza! Mashabiki wachache na wa ukweli watakaoinunua album hiyo, watakuwa wamepewa zawadi muhimu itakayodumu kwa miaka mingi.

Unadhani kwanini hadi leo kuna watu wanamiliki album kama Machozi, Jasho na Damu ya Profesa Jay? Ni kwasababu kupitia album hiyo tunakumbuka maisha ya nyuma kipindi inatoka. Wapo wanaokumbuka vitu vya furaha au vya huzuni lakini vyote vimetunzwa kwenye album hii. Mimi naikumbuka sana album hiyo na pengine ni album bora kabisa kuwahi kutolewa na msanii wa hip hop nchini.

Tunakosa uhondo huu. Tunakosa fursa ya kujua uwezo wa wasanii wetu. Tunakosa kujua yaliyomo mioyoni mwao. Tunanyimwa haki ya kuufaidi muziki wao. Tumechoka kusikiliza single moja moja redioni ambazo wasanii wengi huzitengeneza kwa lengo la kutafuta hits ili wapate show. Utengezaji wa album upo tofauti na ile pressure ya msanii kutengeneza hit ya redioni. Katika album, msanii hupata uhuru zaidi wa kufanya muziki anaoupenda bila kuogopa kama utampa show au utapendwa redioni.

Narudia tena, hakuna sababu yoyote ambayo msanii ataniambia kama kisingizio cha kutotoa album nikamwelewa. Hakuna!

Mimi natafsiri kuwa hii inatokana uzembe na uoga, kutojiamini.

Kila siku tunaona picha za wasanii wakiwa studio usiku na mchana wakirekodi nyimbo. Haya manyimbo yote mnayorekodi mnayapeleleka wapi? Kwasababu kwa mwaka msanii akitoa nyimbo nyingi sana, labda ni tano tu, hizi zingine zinaenda wapi? Mnazisikiliza nyumbani na washkaji na familia zenu tu? Wengine wana nyimbo zinazoweza kutosha album hata tano lakini zimo tu ndani wakiziskiliza wenyewe hadi zimewakinai! Kuna tatizo gani ukichagua nyimbo 20 za maana na kutoa album?

Juzi Alikiba alisema ana takriban album nne zipo tayari. Sasa kwanini asitoe album? Na fanbase yake yote ile naye anahofia album haitouza?

Sasa hivi Instagram kumekucha kwa matangazo. Tunaona jinsi wanavyopromote single zao na show zao. Msanii una followers 200k, 300k, 400k na wengine hadi 500k huwezi kuwashawishi 10k tu wakanunua copy halali?

Mnapoteza opportunity kubwa ya kiuchumi na pia mnawakosea sana mashabiki wenu. Imagine ukitoa album ukauza shilingi 10,000 tu na ukifanikiwa kuuza kopi 10,000 una milioni 100 tayari. Unafanya show wanaingia watu 3000 na zaidi, ukifanya show 10 za aina hiyo huwezi kuuza copy zaidi ya 2000? Suala la kuogopa watu kurudufu CD lishapitwa na wakati. Sio la kuogopwa tena. Stickers/mihuri ya TRA ipo hivyo ni muhimu kuzungumza na mashabiki wanunue kopi halali zenye muhuri wa TRA na kama una mashabiki waaminifu watakusikiliza tu.

Matokeo yake rappers ambao wamekuwa wakinyimwa nafasi redioni ndio wamekuwa wakijichanga na kufanya album au mixtape. Wewe msanii ambaye kila siku una show huna sababu ya kuniambia nikauelewa kwanini hutoi album. Ni uoga tu!

Tunahitaji albums, tumechoka na singles zenu nne kwa mwaka!

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents