Habari

Wataka tume kuchunguza kifo cha mtoto aliyekosa 12,000/-

BAADHI ya wananchi wilayani hapa wameitaka Serikali kuunda tume kuchunguza kifo cha mtoto, Veronica Alfred (7) aliyefariki dunia akiwa katika hospitali ya wilaya hiyo baada ya kunyimwa huduma za matibabu, kutokana na mzazi wake kukosa sh. 12,000 za matibabu.

Na Samwel Mwanga, Maswa


BAADHI ya wananchi wilayani hapa wameitaka Serikali kuunda tume kuchunguza kifo cha mtoto, Veronica Alfred (7) aliyefariki dunia akiwa katika hospitali ya wilaya hiyo baada ya kunyimwa huduma za matibabu, kutokana na mzazi wake kukosa sh. 12,000 za matibabu.


Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa kwa nyakati tofauti, walisema kitendo kilichofanywa na baadhi ya watumishi hao si cha kiungwana na kinawafanya watu kupoteza imani na hospitali hiyo.


Walisema kifo cha mtoto huyo kingeweza kuepukwa lakini kwa kuwa wafanyakazi wa hospitali hiyo wameendekeza pesa wakati wakutoa huduma za matibabu, ndiyo maana vifo visivyo vya lazima kama hivyo vinatokea.


Walisema hata kama wazazi wa mtoto huyo kutokuwa na fedha kwa muda huo kwa ajili ya matibabu wangemtibu na baadaye wangefanya utaratibu wa kupata fedha hizo, ikizingatiwa kuwa mtoto huyo alipata ajali ya kutumbukia katika kisima.


“Hiyo ilikuwa dharura hiyo ni ajali kama zingine kilichokuwa kinatakiwa kufanyika ni kumtibu mtoto huyo na kisha suala la fedha za matibabu zingefuata, lakini kitendo cha kukataa kumtibu mtoto huyo si cha kiungwana hata kidogo,” alisema Bw. Andrew John.


Walisema suala kama hilo halikutakiwa kufanywa na watumishi wa Serikali hasa ikizingatia kuwa wanalipwa mishahara yao kutokana na kodi ya wananchi hao, ambao wanashindwa kuwahudumia hata wanapopata ajali kama hizo.


Waliitaka Serikali kutolifumbia macho suala hilo na kuunda tume mara moja kuchunguza tuhuma hizo, ili kuwabaini watu wote waliohusika na kifo hicho na kuchukuliwa hatua za kinidhamu, vinginevyo watakosa imani na Serikali yao.



Mtoto huyo alifariki dunia Novemba 26 mwaka huu, akiwa katika hospitali ya wilaya hiyo, kutokana na kunyimwa matibabu na wauguzi katika wodi namba sita alimokuwa amelazwa baada ya wazazi wake kukosa sh. 12,000 za matibabu.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents