Habari

Watu 20 wamepatiwa chanjo ya ukimwi

IMEELEZWA kwamba, mpaka sasa jumla ya Watanzania 20 wamepatiwa chanjo ya majaribio ya ugonjwa wa ukimwi kwa njia ya kujitolea.

na Peter Nyanje na Rahel Chizoza, Dodoma

 

 

 

IMEELEZWA kwamba, mpaka sasa jumla ya Watanzania 20 wamepatiwa chanjo ya majaribio ya ugonjwa wa ukimwi kwa njia ya kujitolea.

 

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda, aliliambia Bunge mjini hapa jana kuwa, majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa ukimwi yanaendelea kufanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Kituo cha Utafiti cha Mbeya.

 

Akijibu swali bungeni, Dk. Kigoda alisema hakuna malipo yoyote yanayotolewa kwa watu wanaojitolea kufanyiwa majaribio ya dawa za chanjo za ugonjwa huo.

 

Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wataalam kabla ya kuanza kutolewa kwa chanjo hizo, hakuna athari zozote wanazoweza kupata watu waliopatiwa kinga hizo, kutoka katika vituo vya utafiti nchini, ambako ufuatiliaji wa kisayansi unafanyika, ili kupata chanjo kamili.

 

Aidha, aliwataka Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kuhakikisha kuwa wanapatiwa chanjo za magonjwa kama vile homa ya manjano na uti wa mgongo, kwani sheria inazitaka nchi kuwataka wageni kuwa na chanjo hizo.

 

Alizitaja nchi ambazo ni lazima Watanzania wapatiwe chanjo kabla ya kwenda ni Saudi Arabia ambayo hudai chanjo ya uti wa mgongo na Afrika Kusini ambayo hulazimisha chanjo ya homa ya manjano.

 

Alisema pia watu kutoka nchi ambazo zina magonjwa yanayoweza kuambukizwa hapa nchini, watu wake wanapoingia nchini hutakiwa kupatiwa chanjo na hukaguliwa katika viwanja vya ndege kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

 

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo (CCM), aliyetaka kujua ni magonjwa yapi ambayo hupatiwa chanjo kwa Watanzania wanaosafiri kwenda nje ya nchi na idadi ya watu waliopatiwa chanjo ya kinga ya ukimwi mpaka sasa.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents