Habari

Wauza chips Mbeya wadaiwa kukaangia mafuta ya transfoma

Mamalishe na wauza chips mkoani hapa, wanadaiwa kutumia mafuta ya transfoma kupikia vyakula vya wateja. Kufuatia hatua hiyo, uongozi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) mkoani Mbeya, umeahidi kuchukua
hatua za kisheria

Na Pendo Fundisha, PST Mbeya

 
Mamalishe na wauza chips mkoani hapa, wanadaiwa kutumia mafuta ya transfoma kupikia vyakula vya wateja. Kufuatia hatua hiyo, uongozi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) mkoani Mbeya, umeahidi kuchukua
hatua za kisheria kwa kuwabana wafanyakazi wake wanaodaiwa kulihujumu shirika na kutishia afya za wateja wa vyakula.

 

Meneja wa TANESCO mkoani humu, Bi. Stella Hizza, alisema jana kuwa, uongozi umeamua kuwabana wafanyakazi wasio waadilifu na kulisafisha shirika kutokana na wateja kukosa imani na utendaji wake na pia kuwepo malalamiko ya kuhatarisha afya za wananchi.

 

“Sasa wakati umefika wa kutowalea na kuwaonea aibu baadhi ya wafanyakazi wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli, kuuza mafuta ya transfoma na kutoa lugha chafu na za
kashfa kwa wateja ,“ alisema.

 

Aliongeza kuwa, malalamiko mengi yanayopokewa yanahusu ankara za malipo kutofautiana na kiwango cha matumizi ya umeme, hali inayobainisha kuwa wasomaji mita wamekuwa wakikadiria na si kusoma viwango vya umeme vilivyotumika.

 

Alisema utapeli huo unatokana na kuwepo vibarua wa muda ambao waliajiriwa kwa muda na TANESCO lakini hawana utaalam na pale wanapomaliza mkataba huendelea kufanya kazi kwa siri na kuwaibia wateja.

 

Aliongeza kuwa, wafanyakazi wanaoitwa vishoka na amelalamikiwa kuwa wamekuwa wakijichukulia sheria mikononi na kuwakatia umeme wateja huku wakichelewa kuwarudishia kwa nia ya kutaka kupewa rushwa.

 

Bi. Hizza aliwataka raia wema kutoa taarifa za kuwafichua wale wote wanaotapeli wateja na wanao hujumu mali za TANESCO na kuwahakikishia watakaotoa taarifa hizo siri zitatunzwa na kuzawadiwa.

 

Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Aisha Kigoda, aliliambia Bunge kuwa ulaji wa vyakula vilivyopikwa na mafuta ya transfoma ni hatari kwa afya kwa vile mbali na kuharibu maini, mapafu na ngozi pia husababisha saratani.

 

Alisema ni hatari kula pamoja na kupaka mafuta hayo ambayo ni sumu.

 

Baadhi ya wajasiriamali wanadai kuwa mafuta ya transfoma hufaa kupikia kwa kuwa kiasi kidogo huweza kupikia ama kukaangia chips nyingi tena kwa muda mrefu kwa vile hayaungui kama yalivyo mafuta mengine.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents