Habari

Waziri Simba akaidi kulipia maji

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Sophia Simba, amekuwa miongoni mwa wateja wa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani (DAWASCO), waliong’olewa mabomba katika kampeni yake ya kuwang’olea mabomba wateja wasiolipia ankara zao za maji.

na Hellen Ngoromera

 

 

 

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Sophia Simba, amekuwa miongoni mwa wateja wa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani (DAWASCO), waliong’olewa mabomba katika kampeni yake ya kuwang’olea mabomba wateja wasiolipia ankara zao za maji.

 

Sambamba na Waziri Simba, mwingine aliyeng’olewa bomba lake ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samwel Wangwe.

 

Vigogo hao wawili waling’olewa mabomba yao jana baada ya DAWASCO kufanya ziara ya kuwang’olea mabomba wadaiwa wake katika vituo vya Kawe na Boko, vinavyounganisha maeneo ya Bahari Beach, Kawe Survey na mengine.

 

Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Badra Masoud, Waziri Simba anadaiwa sh 881,499.40 kupitia akaunti yake namba 1946701 ya Bahari Beach, wakati Profesa Wangwe anadaiwa sh 494,025.

 

Badra alisema kutokana na hatua hiyo, shirika hilo litamfikisha mahakamani Waziri Simba kutokana na kukiuka taratibu za DAWASCO.

 

Alisema pamoja na kudaiwa huko, waziri huyo ambaye katika nyumba hiyo inaelezwa kuishi jamaa zake, alikatiwa maji Januari 8 mwaka huu baada ya kampeni hiyo, lakini baadaye alijiunganishia bomba kinyemela.

 

“Mwanzo wa kampeni hii Sophia Simba alikuwa mmoja kati ya wateja tuliowakatia, lakini alijiunganishia kinyemela na kutumia maji kwa wizi, kutokana na kung’olewa bomba hili itabidi aanze upya kuwa mteja wetu,” alisema Badra.

 

Alisema katika zoezi hilo litakaloendelea wiki hii, DAWASCO itawang’olea mabomba wateja 96 katika maeneo hayo ya Boko na Kawe.

 

Aliwataka wateja wake kuwa na ushirikiano na shirika hilo kwa kulipa madeni yao, ili kujiepusha na usumbufu unaoweza kujitokeza kwao.

 

Naye meneja wa shirika hilo eneo la Boko, alisema baada ya kuwakatia maji kwa mara ya kwanza waliwataka wateja wao kwenda kulipia bili zao katika kipindi kisichozidi wiki moja, vinginevyo wangechukua hatua ya kuwang’olea mabomba yao.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Hemed Rajabu, ambaye alidai kuwa ni mfanyakazi wa Waziri Simba, alisema katika nyumba hiyo wanaishi jamaa wa waziri huyo.

 

Sambamba na Waziri Simba, DAWASCO imesema itamchukulia pia hatua za kisheria Profesa Wangwe kutokana na kutolipia ankara yake pamoja na kumiliki laini nne za maji, kitu ambacho si halali.

 

“Ni kosa kwa mteja kuwa na laini zaidi ya moja, lazima Wangwe achukuliwe hatua za kisheria,” alisema Meneja wa DAWASCO wa eneo la Kawe, Donart Taratibu.

 

Wateja wengine waliong’olewa mabomba na kiasi wanachodaiwa kikiwa katika mabano ni Malya Richard (sh 455,842), Sara Malekia( sh milioni 1.6), Jaliya Mayanja ( sh milioni 1.1), Ahmad Ahogwa(sh milioni 1.2) na kampuni ya Radi Services inayodaiwa sh 813,526.75.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents