Martial aomba kuondoka Manchester United
Mshambuliaji wa Manchester United raia wa Ufaransa, Anthony Martial amemwambia kocha wa klabu hiyo, Ralf Rangnick kuwa anataka kuondoka.
Rangnick alisema “alizungumza kwa kirefu” siku ya Jumatano na kijana huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye alimwambia “ni wakati mwafaka wa mabadiliko”.
Martial ameanza mechi mbili pekee za Premier League msimu huu, akifunga mara moja.
Licha ya kutaka kuondoka Old Trafford, Rangnick alithibitisha kuwa klabu hiyo bado haijapokea ofa ya kumnunua fowadi huyo.
Wakala wa mchezaji huyo Philippe Lamboley alithibitisha mapema mwezi huu Martial alitaka kuondoka katika klabu hiyo mwezi Januari, na kuongeza kuwa “atazungumza na klabu hivi karibuni”.
Rangnick alisema: “Alinieleza kuwa amekuwa Manchester United sasa kwa miaka saba iliyopita na anahisi ni wakati mwafaka wa mabadiliko, kwenda mahali pengine.”
Martial alisajiliwa na United mwaka 2015 kutoka Monaco kwa £36m, na kumfanya kuwa mwanasoka ghali zaidi duniani wakati huo.
Amefunga mabao 79 katika mechi 268 akiwa na Mashetani Wekundu lakini amekuwa mchezaji wa pembeni kufuatia kuwasili kwa Cristiano Ronaldo, Edinson Cavani na Jadon Sancho.
Hajashiriki katika mechi yoyote ya Rangnick kama kocha hadi sasa na amecheza mechi 10 pekee katika mashindano yote msimu huu.