Habari

Afisa wa TRA apandishwa kizimbani kisa kumiliki mali zisizolingana na kipato chake

Afisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi amepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kumiliki mali ambazo ni magari 19 na kuishi maisha ya kifahari kinyume na mshahara wake.

Mshtakiwa amesomewa makosa yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi na Wakili wa Serikali, Vitalis Peter ambaye alidai mshtakiwa ana makosa mawili.

Alidai kuwa kati ya March 21, 2016 na June 30, 2016 katika maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa TRA, kama Afisa Msaidizi wa Forodha alikutwa akimiliki mali zisizolingana na kipato chake, kinyume na sheria.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa akimiliki magari 19 ambayo ni Toyota RAV4, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz, Suzuki Carry,Toyota Ipsum, Toyota Wish,Toyota Mark ll, Toyota Regiusage, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Lasso, Suzuki Carry, ambayo yana thamani ya Tsh. Milioni 197.6.

Kosa la pili, anadaiwa kuwa kati ya March 21, 2012 na March 30, 2016 jijini Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA aliishi maisha ya kipato cha juu yenye thamani ya Tsh. 333,255,556.24 tofauti na kipato chake.

Wakili Peter amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo anaomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali (PH).

Hata hivyo, upande wa utetezi kupitia Wakili Elisalia Mosha aliiomba Mahakama hiyo kumpa dhamana mteja wake kwa sababu mashtaka aliyonayo yanadhaminiika kisheria.

Hakimu Shaidi alimtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Tsh. Milioni 20 ambapo alikidhi masharti na kuachiwa huru kwa dhamana.

Kesi imeahirishwa hadi Novemba 7, 2017.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents