Habari

Askofu Gwajima amkanya Halima Mdee, naye ajibu

Baada ya mbunge wa Kawe, Halima Mdee kutuhumiwa kutoa lugha chafu bungeni, hatimaye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemuomba mbunge huyo kumuomba msamaha bungeni Spika wa Bunge, Job Ndugai, kufuatia tuhuma hizo.

Askofu huyo sambamba na kutoa neno la Mungu pia amekuwa akikemea mambo mbalimbali yanayoendelea katika nchi ya Tanzania, pamoja na hivyo aliweza kuzungumzia suala linalomkabili mbunge huyo kwa sasa.

Askofu Gwajima ameyazungumzia hayo Jumapili hii wakati akihubiri kanisani kwake Ubungo jijini Dar es salaam.

“Kwenye bunge kulitokea mbadilishano wa maneno kwenye uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki, inaonekana kuna mahali Chadema hawakutendewa vizuri. Kwenye mabishano hayo mbunge wangu wa Kawe akamwambia spika ‘wewe ni fala.’ Halima hilo jambo si sawa, hilo jambo sio sawa hatuwezi kukemea wengine wewe tukakuacha hilo jambo sio sawa. Ni kweli uliudhika, ni kweli ulikasirika lakini namna ya kuonyesha hasira yako sio kumtukana mtu ambaye ni mtu wa muhimili, ili Tanzania iwe vizuri nenda kaombe msamaha yaishe,”alisema.

“Ni lazima mtu yeyote anayeongoza wananchi awe mfano kwa maneno, vitendo na kwakuwa na moyo wa kuzuia hasira yake. Uwe na uwezo wa kubeba mambo, ukishindwa kujizuia na kumtukana Spika, watoto wanaosikia wanadharau nchi.”

Aidha alisema mbunge huyo kuwa hata kama aliudhika ni afadhali angejiangusha chini na kupiga kelele kuonesha hasira yake na si kutukana. Aliendelea kwa kuongeza kuwa “Koma, acha, wewe ni mbunge mzuri na mimi ni rafiki yako nakuambia ukome kumuambia maneno mabaya Spika.”

Kwa upande wake Mdee amejibu ushauri wa Gwajima kwa kuandika: Namuheshimu sana Mch.Gwajima,sitajibizana nae kwenye mitandao. Niweke rekodi sawa sijamtukana na wala sitarajii kumkosea heshima Spika. Hayo ya J2 namwachia yeye! Yangu na yaliyojiri Bungeni.. Najua jinsi ya kuyahandle. Yawezekana yalishamalizwa kabla ya Ibada yake LEO.

Mdee pamoja na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, tayari wameshahojiwa na Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents