Michezo

Eriksen atuma salamu kwa wachezaji wenzake

Christian Eriksen anaendelea kupata ahueni hospitalini na ametuma salamu zake kwa wachezaji wenzake wa timu ya Denmark.

Eriksen alianguka muda mfupi kabla ya mapumziko katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Euro 2020 ambapo Denmark ilikuwa ikichuana dhidi ya Finland Jumamosi usiku.

Mchezaji huyo wa Inter Milan mwenye umri wa miaka 29 alipata matibabu ya dharura uwanjani kabla ya kupelekwa hospitalini alikolazwa.

“Hali yake ni sawa na anaendelea kulazwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi,” ilisema taarifa ya shirikisho la mpira wa miguu la Denmark.

“Leo asubuhi tumezungumza na Christian, ambaye ametuma salamu zake kwa wachezaji wenzake. Timu na wafanyikazi wa timu ya taifa wamepokea ushauri nasaha baada ya kushuhudia tukio hilo uwanjani na wataendelea kupeana motisha baada ya tukio la jana. Tungependa kumshukuru kila mtu kwa salamu zao za dhati.”

Tukio la Jumamosi lilitokea wakati mpira ulipigwa kuelekea kwa Eriksen karibu na mwisho wa kipindi cha kwanza.

Wenzake waliofadhaika walimzunguka kumpa faragha japo katika hali ile mashabiki katika uwanja wa Parken walionekana kukasirika wakati mchezaji huyo alipotibiwa.

Daktari wa timu ya Denmark Martin Boesen alisema Eriksen alikuwa amepoteza fahamu alipomfikia mchezaji huyo uwanjani.

“Nilipomfikia alikuwa amelala upande, alikuwa akipumua, nilihisi mapigo ya moyo, lakini ghafla hilo ilibadilika na tukaanza kumpa CPR,” alisema.

“Msaada ulikuja haraka sana kutoka kwa timu ya matibabu na wafanyakazi wengine kwa ushirikiano wao, na tulifanya kile tulichopaswa kufanya na kufanikiwa kumrudisha Christian.”

Mwezi uliopita, Eriksen aliisaidia Inter Milan kutwaa taji lao la kwanza la Italia baada ya miaka 11 kupita katika msimu wake wa kwanza.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents