Habari

Kampuni ya LG yafungua duka jipya Posta jijini Dar, Fatema Dewji mshirika

Kampuni ya LG Electronics imesema ina mpango wa kuimarisha uwepo wake katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kufungua maduka mapya katika nchi nne ili kukidhi mahitaji ya wateja wa vifaa vya nyumbani na viyoyozi.

Mkurugenzi wa Masoko kutoka kampuni ya MeTL, Fatema Dewji ambayo ni mshirika wa kampuni ya LG akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa duka hilo.

Kampuni hiyo, ambayo leo Juni 7, 2021 imezindua duka jipya katika mitaa ya Posta karibu na mnara wa saa Jijini Dar es Salaam,imesema miendendo ya wateja inaonesha ongezeko kubwa la uhitaji wa bidhaa zake hapa nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendji wa LG Electronics Afrika Mashariki, Bw. SaNyoung Kim alisema hili ni duka la kwanza jijini Dar kwani dula la pili linatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni katika ukumbi wa Mlimani City.

Kwa mujibu wa Bw. SaNyoung Kim, maduka haya yataimarishwa vilivyo ili kuongeza mauzo na kuwapa wateja nafasi nzuri ya kufurahia teknolojia na bidhaa mpya za kampuni hiyo kama vile TV ya OLED, friji ya InstaView, mashine ya kufulia ya TWINWash, mashine ya kupashia chakula aina ya Neochef na mashine za kufulia yenye nguvu ya AI DD AI.

“Posta na Mlimani City ni maeneo mwafaka kabisa kwa sababu ya wateja wengi wanatembelea maeneo hayo na tumejionea namna mazingira ya biashara Tanzania yalivyochangamka. Tunaahidi kuwapa wateja wetu huduma na bidhaa nzuri ili wajisikie fahari wakati wanafanya manunuzi kwani watahudumiwa na wafanyakazi wetu wenye utaalamu wa hali ya juu,” alisema Kim, huku akiwaomba Watanzania watembelee maduka hayo mawili ili
wajionee wenyewe.

Kuhusu kufungua maduka mengine mikoani, Meneja Masoko na Mauzo wa Kampuni hiyo, David Kessy alisema kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara katika soko la vifaa hivyo, wanafikiria kufungua maduka mikoani katika siku za usoni.

“Katika miaka michache iliyopita, tumekuwa tukitanua wigo na uwepo wetu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Tuna mpango wa kuendelea kukuza bidhaa zenye hadhi ya premium na kuwapa wateja wetu bidhaa wanazotarajia wao binafsi na kama biashara kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa zaidi ya daraja la kwanza,” alisema Kessy.

Kessy alisema mauzo ya vifaa vya umeme yameongezeka kutokana na wateja wengi kununua vifaa vya kiteknoojia zaidi kwa matumizi ya nyumbani na pia kwa masomo, mapishi na burudani.

“Ni wazi kuwa wakati huu wa janga la Corona, teknolojia imekuwa muhimu sana katika maisha ya watu huku tukishuhudia uvumbuzi mbalimbali ambao unaendana na ufanisi na afya bora,” aiongeza Kessy.

Alisema LG kwa sasa inasambaza vifaa vya hadhi ya premium vyenye uwezo wa kutumia nishati kidogo katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuhakikisha utunzaji wa mazingira na rahisi kutumia.

Mwaka jana, LG ilizindua maduka maalumu ya mtandaoni nchini Kenya ili kukidhi mahitaji ya wateja wanaopendelea kununua vifaa vya umeme kwa njia ya mtandao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents