Habari

Mgomo wawagawa wanafunzi Muhimbili

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUCHS) jana walitangaza kuanza mgomo wakipinga wenzao wa mwaka kwa kwanza kukaa nyumba za kulala wageni wakati kuna hosteli mpya zilizopo Masaki, wamejikuta wakigawanyika katika makundi.

na Adili Gurumo, IUCO na Mobini Sarya


WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUCHS) jana walitangaza kuanza mgomo wakipinga wenzao wa mwaka kwa kwanza kukaa nyumba za kulala wageni wakati kuna hosteli mpya zilizopo Masaki, wamejikuta wakigawanyika katika makundi.


Mgawanyiko huo unatokana na tangazo lililotolewa juzi na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kisali Palangyo, kuwa atakayeshiriki katika mgomo huo atachukuliwa hatua kali kulingana na taratibu za chuo.


Kutokana na hali hiyo, baadhi yao walikaa chuoni hapo, ili kukwepa kuingia katika mtego wa upande mmoja, wakati wengine waliofika walionekana kutawanyika makundi mawili na wengine kuingia na wengine kubaki wakizunguka katika viunga vya chuo.


Rais wa Serikali ya Wanafunzi (MUHASSO), Edwin Chitage, alisema lengo la mgomo huo ni kuushinikiza uongozi wa MUCHS kuwapa ruhusa ya kuhamia katika hosteli za Masaki wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 24 kwa sasa wanaoishi katika nyumba za wageni maeneo ya Magomeni.


Chitage alisema hosteli hizo zimekarabatiwa kwa sh bilioni1.2 zaidi ya miaka saba iliyopita, lakini wanafunzi wanaishi katika mazingira magumu huku uongozi ukitoa visingizio visivyo na maana, kwamba hakuna fedha za kununulia vitanda na pamoja na kujenga kantini ya chakula.


Alikanusha madai kwamba chuo hakina fedha za kumalizia ukarabati na kueleza kuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia iliwahi kuiambia MUCHS ichukue sh milion 156 za ukarabati, ili iwape wanafunzi wanaotaka kwenda mafunzo kwa vitendo.


Akizungumza na waandishi wa habari, Profesa Palangyo alisema kwamba hakuna mgomo wowote chuoni hapo na kudai kuwa wanaoeleza kuwapo kwa mgomo ni viongozi wa wanafunzi. Alionya wale wanaowasumbua wanafunzi watachukuliwa hatua.


Hata hivyo, hali chuoni hapo inaonekana kuwapo kwa mgomo kutokana na pia bango lililowekwa na wanafunzi linalosema ‘hakuna madarasa na mgomo unaendelea hadi kieleweke’, huku bango lililowekwa na uongozi wa chuo likieleza ‘masomo yanaendelea kama kawaida asiyeingia vipindi havitarudiwa, anayetaka kuingia darasani aingie ulinzi utakuwapo wa kutosha”.


Akielezea kuhusu Hosteli mpya zinazodaiwa kutotumika, alisema bado zina upungufu mkubwa kwani hakuna ulinzi, hakuna vitanda wala magodoro, mifereji ya kupitisha maji machafu na sehemu ya kulia chakula, suala alilosema linachangiwa na kukosekana kwa fedha za kumalizia.


Hata hivyo, Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Hellen Mtuli, alisema wameshapata mkandarasi wa kutengeneza vitanda na magodoro, wanachosubiri ni wizara iwalipe deni lao na kwamaba wameunda kamati itakayotoa mapendekezo ya kiasi cha gharama zinazohitajika kukamilisha ukarabati huo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents