Habari

‘Wafadhili wanatukwamisha’

WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Hussein Mwinyi amesema kutokamilika kwa baadhi ya miradi inayofadhiliwa na wahisani kunasababisha hali ya uchonganishi baina yao na Serikali za Mitaa.

Shadrack Sagati, Kibaha


WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Hussein Mwinyi amesema kutokamilika kwa baadhi ya miradi inayofadhiliwa na wahisani kunasababisha hali ya uchonganishi baina yao na Serikali za Mitaa.


Dk. Mwinyi aliyasema hayo mjini hapa jana katika mazungumzo na viongozi na watendaji wa Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani katika mfululizo wa ziara za mawaziri na manaibu wao mikoani zinazomalizika leo.


Alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya watendaji kusema fedha wanazopangiwa katika bajeti hawazipati zote.


Walisema hali hiyo inachangia miradi mingi kutokamilika na hivyo kutafsiriwa na wananchi kuwa watendaji wanakula fedha za umma. “Hili ni tatizo na naomba mawaziri hili mtusaidie,” alisema George Lugome ambaye ni mchumi wa halmashauri.


Akijibu hoja hiyo, Dk. Mwinyi alikiri kuwa kuna tatizo hilo na linatokana na fedha za wahisani kuwa na masharti na wakati mwingine hawatoi zote. “Wao wana masharti usipotekeleza hayo wanabana fedha na halmashauri zinakosa,” alisema.


Aliahidi kufikisha tatizo hilo Hazina na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ili lishughulikiwe na miradi iliyopangwa itekelezeke.


Mapema, Mbunge wa Kibaha, Dk. Zainab Gama (CCM) alishauri mawaziri wanaozuru mikoani kufafanua tuhuma za ufisadi zinazotolewa na wapinzani kwa kile alichodai kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wanaziamini.


Mbunge huyo alisema kama mawaziri watazifafanua tuhuma hizo pamoja na bajeti itakuwa rahisi kwa viongozi wa CCM kuzijibu katika ngazi zao za uongozi.


“Wananchi wameanza kuwaamini … tufanye utaratibu wa kuzijibu na kufafanua kwa wananchi,”
alisema alipohutubia katika mkutano mjini Kibaha ambao Dk. Hussein Mwinyi pia alihutubia.
Akizungumzia tuhuma hizo, Dk. Mwinyi aliwataka viongozi wa CCM kutumia taarifa ya serikali kuzijibu tuhuma hizo.


“Serikali imekwisha kujibu tuhuma za BoT na Buzwagi kupitia vyombo vya habari. Sina haja ya kufafanua zitumieni hizo kujibu mapigo,” alisema na kuongeza kuwa wapinzani wanapotosha bajeti katika suala la kodi ya mafuta ndiyo maana mawaziri wamelazimika kwenda kwa wananchi kufafanua hali halisi ya bajeti na ubora wake.


Naye Merali Chawe anaripoti kutoka Mbozi kwamba baadhi ya wakazi wa Ileje na Mbozi Mkoani Mbeya wameilalamikia serikali kuwa fedha za Mikopo ya wajasiriamali katika mwaka mmoja uliopita zimewanufaisha watu wenye kipato cha juu tu wakiwamo wafanyabiashara na wafanyakazi na kuwatenga wananchi wa vijijini hasa wakulima.


Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti na wananchi hao wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Rita Mlaki.


Akizungumza katika mkutano uliowahusisha watendaji wa wilaya na madiwani, Gidion Mkondya alisema kuwa vyama vya akiba na mikopo vilinufaika na fedha hizo ni vile vilivyoanzishwa na wafanyakazi na wafanyabiashara.


Mkondya alisema kuwa wakulima ambao wamekuwa wakitegemea kipato mara moja kwa mwaka baada ya mavuno, wamekuwa hawanufaiki na mikopo hiyo kwa kuwa hakuna aliye tayari kuwakopesha kutokana na kutokuwa na uhakika wa fedha zao kurudi.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Mlaki aliwataka maofisa maendeleo ya jamii kuwasaidia wananchi wa vijijini kuanzisha na kuzisajili Saccos zao ziweze kunufaika na fedha za mikopo zinazotolewa na taasisi mbalimbali za fedha.


Alisema wananchi wa vijijini wanaweza kudhani wanatengwa na serikali kwa kutopata fedha hizo za mikopo, lakini kutokana na kutojua taratibu za uanzishaji wa Saccos na uombaji wa mikopo wengi wamekuwa wakishindwa kupata fedha hizo.


Katika mikopo iliyokuwa ikizungumzwa, Mkoa wa Mbeya ulipata Sh bilioni 4.7 na Wilaya ya Ileje ilipata Sh milioni 29 na watu 55 walijitokeza kukopa.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents