Burudani

Sababu za kuchelewa kutangaza majina yaliyoingia kwenye Top 5 ya tuzo za watu 2015

Tunapenda kuwaomba radhi wananchi kwa kuchelewa kutangaza majina yaliyoingia kwenye hatua ya tano bora katika vipengele 14 vinavyoshindaniwa kwenye Tuzo za Watu 2015. Hii imetokana na sababu mbalimbali ambazo zimekuwa nje ya uwezo wetu.

square_with_sponsors small

Sababu hizo ni pamoja na:

1. Zoezi la kukusanya na kuhesabu mapendezo kuwa refu kutokana na wingi wa kura kuliko ilivyotarajiwa

Mwaka huu muitikio kwenye tuzo za watu umekuwa mkubwa kiasi ambacho mapendekezo yaliyotumwa yamekuwa mengi kuliko matarajio yetu. Kwakuwa tupo makini katika kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa kila aliyependekeza na kupendekezwa, zoezi la kuhesabu mapendekezo hayo kupata majina hayo limechukua takriban siku tatu. Mwaka jana hali ilikuwa tofauti kidogo kwakuwa zoezi hilo lilichukua muda wa siku moja peke yake.

2. Ukaguzi wa filamu na video za muziki zilizopendekezwa

Kwakuwa tuzo za watu zinazingatia viwango vya kila washiriki kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania, filamu tano zilizoingia kwenye kipengele cha filamu inayopendwa pamoja na video zilizoingia kwenye kipengele cha video ya muziki inayopendwa, ziliwasilishwa kwenye bodi ya filamu Tanzania pindi tu zoezi la kukusanya mapendekezo hayo lilipomalizika. Bodi hiyo ilizikagua filamu na video hizo na kuziwekea makundi mbalimbali kufuata maudhui na rika linalotakiwa kuziona na kama ishara kuwa zimeruhusiwa kuonekana kwenye umma ya Tanzania.

3. Ukaguzi wa mapendekezo hayo na mamlaka iliyopewa dhamana

Mwaka huu kura zote zinazopigwa zinakaguliwa na kampuni ya masuala ya hesabu iitwayo Deloitte ili kuhakikisha kuwa washindi wanapatikana katika mazingara ya haki na ya wazi zaidi. Hivyo kampuni hiyo imekabidhiwa mapendekezo hayo kama yalivyokusanywa na kuchambuliwa kwa ushirikiano wa baraza la sanaa Tanzania, BASATA na Bongo5. Deloitte ikimaliza kufanya ukaguzi katika kipengele kulingana na majina matano yaliyopendekezwa zaidi na kwa kufuata vigezo vilivyowekwa, majina hayo yatatangazwa rasmi.

Zoezi hilo linatarajiwa kumalizika Jumatano au Alhamis hii na ndipo tutakapotangaza majina ya tano bora.

Ni matumaini yetu mtatuwia radhi kwa kuchelewa kutangaza majina hayo lakini pia mtaelewa sababu ya kufanya hivyo na kwamba lengo ni kuhakikisha kuwa Tuzo za Watu zinakuwa ni tuzo halali na makini zaidi.

Asanteni.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents