Habari

Shirika la Usafirishaji Dar es salaam (UDA) kuleta mabasi 2000 maalum kwaajili ya wanawake

Habari njema kwa wanawake wakazi wa Dar es salaam ni kuwa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam, (Uda) linatarajia kuleta mabasi yapatayo 2000 yatakayokuwa yakitoa huduma za usafiri kwa wanawake tu jijini Dar es salaam.

Robert Kisena
Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena

Kwa mujibu wa NIPASHE, Kampuni ya Simon Group, imekabidhi mabasi 40 kwa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam, (Uda) ili kurahisisha usafiri Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe ya uzinduzi wa mabasi hayo jijini Dar es Salaam, jana Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena, alisema huo ni mpango wa muda mfupi wa uwekezaji na uendelezaji katika shirika la Uda, lengo ikiwa ni kuingiza mabasi mapya mengine 2000 ifikapo Juni, 2014.

“Katika mabasi hayo, pia kutakuwa na mabasi maalum ya kubeba wanawake pekee, lengo la kuwa na mabasi haya, ni kuwapunguzia usumbufu akina mama wa Dar es Salaam, ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiteseka kupigana vikumbo na wanaume katika kugombania usafiri wa maeneo mbalimbali hapa jijini,” alisema Kisena.

Kisena alisema vile vile Uda limeingia ubia na Kampuni za Africarriers na Eicher wa kununua mabasi hayo 2,000 ifikapo Juni mwakani.

Kisena aliongeza kuwa huo ni mpango wa muda mfupi wa uwekezaji na uendelezaji wa Uda wenye nia ya kuboresha huduma ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ambapo katika mpango wa muda mrefu ni kuingiza magari mengine 5,000 na kufikisha idadi ya magari 7,000 ifikapo mwaka 2017.

SOURCE: NIPASHE

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents