Habari

Sijapiga ‘stop’ mashindano ya Miss Tanzania wala tuzo za muziki – Waziri Mwakyembe

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametolea ufafanuzi kauli yake na kusema kuwa hajasitisha mashindano ya Miss Tanzania na tuzo za muziki nchini bali ametoa angalizo kwa waandaaji wa mashindano hayo kuwa na uhakika wa kuyaendesha.

Dk Mwakyembe amesema hayo hii Jumatatu kwenye ziara yake mjini Mtwara baada ya taarifa kuenea kuwa amefuta shindano hilo.

Mwakyembe yuko mkoani Mtwara katika ziara ya kuzungumza na watendaji walio chini ya wizara yake na kuzungukia viwanja vya michezo.

Amesema mashindano na tuzo hapa nchini huanzishwa bila kuwa na andiko la uendelezaji, hivyo ametoa agizo kwa Baraza la Sanaa (Basata) kwamba mtu yeyote akija na shindano au wazo la tuzo watamruhusu pale tu atakapotoa msingi wa mwendelezo na siyo kwa kuwa amepata mfadhili wa muda.

“Hata mashindano ya ulimbwende tumeshachoka watoto wa kike wanahangaika, watajipodoa lakini zawadi zikitangazwa unaambiwa mshindi wa kwanza gari namba mbili pikipiki ila sijawahi kuona hata mmoja ambaye amewahi kuzipata au ikatokea utoaji wa zawadi usio na kelele,” amesema.

Dk Mwakyembe amesema amekuwa akifuatwa na warembo kadhaa ofisini kwake wakilalamikia kutopewa zawadi zao mara baada ya mashindano ya Miss Tanzania, amesema alikaa na Basata miezi miwili iliyopita na kuwapa maagizo, “Kuanzia sasa chombo chochote au kampuni inayoendesha mashindano ya ulimbwende ambayo iliwahi kuahidi vijana wetu wa Kitanzania zawadi na haijatoa tusigombane, watoe zawadi zote wawatafute warembo wawape.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents