Michezo

Simba wamruhusu Buswita kujiunga Yanga kwa masharti

Kamati ya hadhi na haki za wachezaji ya TFF, imetangaza kuafiki makubaliano ya Simba na Yanga kuhusu mchezaji Pius Buswita ambaye alifungiwa kwa kusaini mikataba ya kuzitumikia klabu hizo ndani ya msimu mmoja, kwa wekundu wa Msimbazi kumruhusu kujiunga na watani wao wa jadi,

Pius Buswita

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dare se salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji, Elias Mwanjala, amesema kamati yake imefikia uamuzi huo baada ya klabu hizo mbili kufikia makubaliano na kuyafikisha kwenye kikao chao kilichofanyika mwanzoni mwa wiki hii.

Mwanjala amesema kuwa kamati yake imemfungulia Buswita, lakini haitamruhusu kuanza kucheza mpaka pale Yanga itakapokuwa imeilipa Simba fedha hizo ambazo mchezaji huyo alilipwa na mabingwa hao wa Kombe la FA.

Hata hivyo, Mwanjala amesema kamati yake itamuandikia barua ya onyo kali Buswita kutokana na kosa ambalo amelifanya, ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine na kueleza kwamba hatua kali zingechukuliwa endapo Simba na Yanga ambazo zinadhaminiwa na Kampuni ya Kubeti ya SportPesa, zingeshindwa kukubaliana nje ya kamati hiyo.

Kikubwa pia, kamati yetu inataka kuona mchezaji anacheza na si kufungia fungia watu, lakini hii imetokana na Yanga kukubali kulipa deni ambalo Simba ilifikisha malalamiko yake na mchezaji mwenyewe alikiri alichukua pesa, na pia tungeliacha, Simba wangeweza kuchukua hatua nyingine zaidi ambazo zingekua hatari kwa mchezaji, ingawa walikiuka taratibu za usajili,” amesema Mwanjala.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kamati yake imetoa muda wa wiki mbili kwa klabu zote ambazo zimekutwa na hatia ya kudaiwa malimbikizo ya mishahara na wachezaji na madeni ya ada za uhamisho kukamilisha ndani ya wiki mbili na wale ambao hawatatekeleza, watakatwa fedha zao kupitia Bodi ya Ligi.

SOMA ZAIDI – Shetani alinipitia nikasaini  Simba na Yanga – Buswita

Pia alizitaka klabu zote hapa nchini kuwasilisha nyaraka za mikataba yao na wadhamini kabla ya kusainiwa, ili kupata ushauri wa kisheria ambao utalenga kuzilinda pale inapotokea mikataba hiyo kuvunjika “kihuni” na kusababisha wachezaji kuathirika.

Hapa napenda kutoa mfano kwa Stand United ambao waliingia mkataba na Acacia, baada ya wadhamini hao kuondoka, klabu imebaki kwenye madeni ambayo awali waliweza kuyamudu wakiwa na mdhamini huyo,” amesema Mwanjala .

Buswita alisaini Simba mkataba wa awali na kuchukua kiasi cha shilingi milioni 10 za Tanzania na baadae akasaini na Yanga, kitendo ambacho ni kinyume na kanuni za usajili kwa mchezaji mmoja kusaini timu mbili, kitendo ambacho kilipelekea aadhibiwe kwa kufungiwa kucheza soka kwa mwaka mmoja.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents