Habari

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yawataka wanasiasa kutumia mahakama kudai haki zao

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), imewataka wanasiasa nchini wanaonyimwa haki za kufanya mikutano kwenda mahakamani kwa ajili ya kudai haki hiyo ambayo ipo wazi katika misingi ya sheria na Katiba ya nchi.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Tom Nyanduga.

Hayo yamesemwa jana jumanne na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Tom Nyanduga, wakati wa mkutano ulioikutanisha Tume hiyo na asasi za kiraia uliolenga kufanya tathmini ya Tanzania katika utekelezaji wa mapendekezo ya Baraza la Kimataifa la Haki za Binadamu (UPR) kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo imekubali kuitekeleza.

Nyanduga amesema vyama vya siasa vinatambua fika kuwa Katiba imeeleza kwa kina kuhusu mikusanyiko inapotokea kuna ukiukwaji, Mahakama ndiyo sehemu sahihi ya kukimbilia.

Haki ya mtu inapopokwa sehemu ya kukimbilia ni mahakamani na wanasiasa wanajua hilo. Hili suala si la kuiachia Tume peke yake, vyama vya siasa vinatambua fika haki hiyo ambayo iko wazi kisheria kama ilivyoainishwa kwenye ibara 26(b) ya Katiba inamtaka kila Mtanzania kulinda Katiba.“amesema Nyanduga.

Kwa upande mwingine, Mhadhiri katika Shule ya Sheria, Dk James Jesse akitilia mkazo suala hilo amesema licha ya Tanzania kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu, kumekuwepo na malalamiko mengi ya ukandamizaji wa uhuru wa kutoa mawazo na mikutano ya kisiasa.

Dk Jesse amesema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuzuia mikutano ya kisiasa una nia njema ya kuwafanya Watanzania wajikite zaidi kwenye kazi lakini uhuru wa watu kuzungumza unapaswa kuzingatiwa na kupewa kipaumbele.

Nia ya Rais ni nzuri ana maana watu wasipoteze muda mwingi kufanya siasa badala yake wafanye kazi lakini lazima kuwe na kiasi. Bila kufanyika mikutano watu wanawezaje kuelezea changamoto zao au kukosoa vitu ambavyo haviko sawa,” amesema Dkt Jesse kwa kuhoji huku akiendelea kwa kusema kuwa

Ni kweli mikutano inaweza kupunguzwa lakini si kuizuia kabisa kwa kuwa ndiyo afya ya vyama vya siasa, itawezekana vipi kwa vyama kupata wanachama wapya endapo hakutakuwa na mikutano. Hata hili suala la kuzuia wabunge wasifanye mikutano nje ya majimbo yao sioni kama ni sawa. Tathimini imeonyesha kuna malalamiko mengi yanayohusu uhuru wa kutoa mawazo kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii.”amesema Dkt. Jesse.

Hata hivyo, Dkt. Jesse alizungumzia kuhusu uhuru wa Vyombo vya Habari akisema kuwa tathmini imeonesha kuna vitendo vinavyoendelea na kuashiria ukandamizaji wa uhuru wa kupata na kutoa habari.

Chanzo:Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents