Habari

Wahanga wa Tabata Dampo kuhamishiwa..

Familia 96 za wahanga waliobomolewa nyumba zao `kitatanishi` katika eneo la Tabata Dampo, Dar es Salaam, watahamishiwa Shule ya Msingi Kipawa, mvua za masika zitakapoanza kunyesha wakati wowote kuanzia sasa.

Na Grace Chilongola, PST

 

 

 
Familia 96 za wahanga waliobomolewa nyumba zao `kitatanishi` katika eneo la Tabata Dampo, Dar es Salaam, watahamishiwa Shule ya Msingi Kipawa, mvua za masika zitakapoanza kunyesha wakati wowote kuanzia sasa.

 

 

 

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Bw. John Lubuva wakati Kamati ya Mipango miji, fedha na utawala ya manispaa hiyo zilipofanya ziara kwenye eneo la wahanga pamoja na iliyokuwa Shule ya Msingi Kipawa.

 

 

 

Bw. Lubuva alisema madarasa ya shule hiyo hivi sasa yanatumiwa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Vingunguti ambapo Shule Sekondari ya Vingunguti bado haijakamilika.

 

 

 

Alisema katika kuwanusuru wahanga hao waliobomolewa nyumba zao na mvua, wanafunzi hao watahamishiwa katika Shule ya Msingi ya Uhuru mchanganyiko ili kuwahifadhi wahanga hao.

 

 

 

Alisema wanafunzi wanaosoma katika shule ya Uhuru Mchanganyiko watahamishiwa katika shule ya Gerezani.

 

 

 

Kwa muda mrefu majengo ya Shule ya Msingi Kipawa yalikuwa hayatumiki baada ya eneo hilo kuthaminiwa kwa ajili ya kupisha eneo la Uwanja wa Ndege ambapo wakazi wake tayari walikwishalipwa fidia.

 

 

 

Kamati hizo zilipata nafasi ya kutembelea viwanja vilivyopimwa na serikali eneo la Buyuni kata ya Chanika ambako manispaa imetenga viwanja 96 kwa ajili ya wahanga hao.

 

 

 

Katika ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Bw. Abuu Jumaa, aliwakabidhi wahanga hao katoni 10 za sabuni, sembe viroba 10, mchele viroba 10 na katoni 50 za maji.

 

 

 

Akikabidhi msaada huo, Meya Jumaa alisema wamekuwa wakilifuatilia suala hilo kwa karibu, na kwa kuwa lipo kwenye tume hawana la kusema bali ni kuangalia hali halisi huku wakisubiri mapendekezo ya tume iliyoundwa na serikali.

 

 

 

Hivi karibuni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), iliunda tume ya watu wanne kuchunguza bomoabomoa hiyo yenye utata.

 

 

 

Tume hiyo ilifutilia mbali tume nyingine iliyokuwa imeundwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilionekana machoni mwa watu kama kiini macho kwani Manispaa hiyo ndio inayolaumiwa kwa kuendesha bomoabomoa hiyo bila kufuata taratibu na sheria.

 

 

 

Mwanasheria wa TAMISEMI, Bw. Selestine Nchimbi ndiye mwenyekiti wa tume hiyo wakati katibu wake ni Abraham Shamumoyo na wajumbe wengine ni Mabwana Salum Chima na Joseph Shewiyo, ambaye ni Kamishina Msaidizi wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 

 

 

Tume hiyo imekabidhiwa hadidu za rejea za kuchunguza uhalali wa zoezi zima la kuwabomolea wakazi hao nyumba zao na kuharibu mali bila fidia.

 

 

 

Pia itachunguza kuona kama kanuni, sheria na taratibu zilifuatwa kikamilifu na pia itapitia kwa ufasaha hukumu iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents