Habari

Waliofanyiwa majaribio ya dawa za Ukimwi wanaweza kudai fidia

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema Watanzania 64 waliofanyiwa majaribio ya dawa ya ukimwi iitwayo Virodene Po 58 kinyume cha utaratibu wana haki ya kudai fidia.

Shadrack Sagati, Dodoma

 

 

 
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema Watanzania 64 waliofanyiwa majaribio ya dawa ya ukimwi iitwayo Virodene Po 58 kinyume cha utaratibu wana haki ya kudai fidia.

 

 

 

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda alisema kama itaonekana Watanzania hao wanahitaji kupata fidia wanatakiwa wafuate taratibu zilizopo ili waende kwenye vyombo vya sheria.

 

 

 

Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu Dk. Wilbrod Slaa (Chadema) ambaye alitaka kujua hatua zinazoweza kuchukuliwa na Watanzania hao dhidi ya wahusika.

 

 

 

Awali alijibu swali la msingi la Dk. Slaa aliyetaka kujua serikali inasema nini juu ya jambo hilo na ni chombo gani cha sheria kilitoa kibali cha majaribio ya aina hiyo kufanyiwa Watanzania.

 

 

 

Dk. Aisha alisema kwa kwaida vyombo vya sheria vinavyohusina na utoaji wa vibali vya utafiti kama huo ni Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR),Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) na COSTECH.

 

 

 

Alisema hata hivyo hakuna hata moja ya taasisi hizo iliyowahi kutoa vibali kwa ajili ya utafiti huo.

 

 

 

Dk. Aisha alisema kumbukumbu zinaonyesha ya kuwa ombi la kibali cha kufanya utafiti liliwasilishwa NIMR Julai 2000.

 

 

 

Alisema hata hivyo baada ya kufanya tathimini ya utafiti huo NIMR ililikataa ombi hilo kwa kuwa andiko kuhusu utafiti wa dawa hiyo lilikuwa na upungufu mkubwa wa kisayansi na maadili.

 

 

 

Dk. Aisha alisema kulingana na maelezo hayo ni dhahiri kuwa majaribio ya Virodene Po 58 kwa Watanzania hao yalifanyika kinyume na taratibu za utafiti.

 

 

 

Alisema baada ya kukataliwa kwa ombi la kufanya utafiti wanasayansi hao waliingiza dawa bila kibali cha serikali na kuanza kufanya utafiti Jeshini Lugalo na wakati huohuo kuziuza dawa hizo holela.

 

 

 

Dk. Aisha alisema baada ya kutambua hali hiyo Agosti 2001 Wizara yake ilitoa agizo la kusimamisha utafiti huo pamoja na kuwafukuza watafiti, wahalifu, kuzuia uingizwaji wa dawa hizo na kuzirejesha zilipotoka.

 

 

 

Alisema wizara yake itajitahidi kuongeza uwezo wa taasisi hizo, kuchunguza tafiti mbalimbali zinazofanywa nchini kuhusu dawa na magonjwa ili kuhakikisha kwamba utafiti wote unafanywa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

 

 

 
Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents