Habari

Wanafunzi watakiwa kutumia teknolojia za mapinduzi ya nne ya viwanda

WANAFUNZI wanaofanya gunduzi na tafiti zenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali katika jamii wametakiwa kujikita zaidi katika kutumia teknolojia zinazoendana na mapinduzi ya nne ya viwanda ikiwa ni pamoja na matumizi ya akili bandia hali itakayowasaidia kuongeza umahiri na kuweza kulinda nafasi zao za ajira.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Mwanzilishi Mwenza wa Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (YST), Gozibert Kamugisha wakati akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari na kuongeza kuwa shirikisho hilo limefanya juhudi za kuwaandaa vijana vijana wanaosoma shule za sekondari kuwa washiriki imara wa mapinduzu hayo.

Alisema jitihada za kuboresha ujuzi wa kisayansi na teknolojia kwa vijana imekuwa kipaumbele cha YST kwa kipindi cha miaka 13 iliyopita na kwamba kupitia mpango wao wa mafunzo shuleni wamekuwa wakiwapatia vijana ujuzi wa kubaini matatizo ya kimaendeleo kwenye jamii zao na kubuni njia za kisayansi kukabiliana nayo.

Aidha Kamugisha alisema kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanafunzi kujihusisha na tafiti za kisayansi na ugunduzi nchini, ambapo kwa mwaka 2023 wanafunzi takribani 979 wamewasilisha maombi, kati yao tafiti 361 zimekubaliwa kuendelezwa chini ya washauri wa kisayansi wa YST.

“Baadhi ya gunduzi na tafiti hizo za kisayasi zitakazoonyeshwa kwenye maonyesho ya mwaka huu ambayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 7, 2023 na yatajikita katika masuala ya utunzaji wa mazao ya kilimo, mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali maji, uzalishaji wa umeme hivyo tunawataka wadau na jamii kwa ujumla kuwaunga mkono wanafunzi hao,” alisema Kamugisha

Naye Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Caren Rowland alisema kuwa taasisi hiyo imeendelea kuboresha programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao ili kuendana na sera ya nchi katika kuleta maendeleo endelevu kupitia uboreshwaji wa miundombinu ya elimu.

“Tumekuwa wafadhili kwa taasisi tofauti tofauti hapa nchini lakini pia tumekuwa tukikuza sayansi na vipaji vya vijana kwa takribani miaka 13 sasa, tutaendelea kuwasapoti YST katika maonesho yao na wanafunzi walionesha ufumbuzi kwa kubuni vitu mbalimbali, ” alisema Rowland

Hata hivyo alisema YST ni msingi wa mpango wa kujenga uwezo ambao unahimiza ari ya kitaaluma na hutoa fursa zinazohitajika za tafiti za kisayansi kwa shule za sekondari Tanzania.

Written by @janethjv255

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents