Habari

Waziri Karamagi atetea mkataba wa Buzwagi

WIZARA ya Nishati na Madini imeeleza kushangazwa kwake na mjadala unaoendelea juu ya mradi wa Buzwagi. Imesema huo ni mkataba ulioboreshwa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mingine iliyowahi kusainiwa.

Stella Nyemenohi


WIZARA ya Nishati na Madini imeeleza kushangazwa kwake na mjadala unaoendelea juu ya mradi wa Buzwagi. Imesema huo ni mkataba ulioboreshwa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mingine iliyowahi kusainiwa.


Katika kile ambacho Waziri Nazir Karamagi alikieleza jana kuwa wapinzani wameamua kutumia mradi huo kama hoja ya kujiegemeza katika siasa, alisema mkataba huo una maeneo mengi yaliyofanyiwa maboresho kwa maslahi ya nchi.


“Mkataba huu hauna tofauti na ile ya zamani; labda upya wake ni kwamba huu ni mkataba bora uliofanyiwa marekebisho makubwa….. wapinzani hawana hoja, wanatafuta mahali pa kuegemea,” alisema Karamagi.


Karamagi, ambaye hata hivyo hakuweza kubainisha kama nakala ya mkataba iliyosambazwa juzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni sahihi au la, alisema hakuna kitu kigeni kilichojitokeza katika mkataba huo. “Huo mkataba waliosema watasambaza sijauona kwa hiyo siwezi kufahamu kama ndiyo wenyewe au la,” alisema Karamagi alipozungumza na HabariLeo kwa simu.


Hata hivyo, alisisitiza kuwa ipo taarifa rasmi ya serikali itakayotolewa wiki ijayo kuelezea uwazi wa mkataba huo na vipengele mbalimbali vilivyoboreshwa ikilinganishwa na mikataba iliyopita ya namna hiyo. Miongoni mwa vipengele vilivyomo katika mkataba huo ni kipengele cha urudishaji wa mitaji ya uwekezaji.


Wakati awali gharama ilikuwa ni asilimia 100 kwa mwaka wa kwanza, mkataba wa sasa unaonyesha kuwa urudishwaji huo utakuwa ni asilimia 80 kwa mwaka wa kwanza na baadaye, miaka inayofuata ni asilimia 50. Vile vile, ndani ya mkataba huo, yapo masharti kuhusu kununua bidhaa na huduma mbalimbali, kwa wawekezaji kutakiwa kuzingatia hilo kwa kununua bidhaa za hapa nchini. Kipengele kingine ni masharti kuhusu kuchangia Mfuko wa Uwezeshaji kupitia Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji wa dola za Marekani 125,000 kwa mwaka.


Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya maofisa wa serikali walisema viongozi wa upinzani wametumia udhaifu wa serikali wa kutokuweka bayana sera mbalimbali zinazotengenezwa kwa ajili ya wananchi.


“Ukikaa na kuchunguza madai ya wapinzani, hupati hoja ya msingi. Cha zaidi, wamewateka wananchi kwa mawazo kwa kutumia udhaifu wao wa kutokuelewa sera na michakato mbalimbali inayoandaliwa kwa ajili yao,” alisema ofisa mwandamizi wa serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe.


Ofisa huyo alishauri badala ya serikali kujibizana na wapinzani hao, iandae utaratibu wa kuwashirikisha wananchi kufahamu sera mbalimbali zilizotengenezwa kwa ajili yao kuepusha kutekwa na watu wenye ajenda binafsi za kutafuta madaraka.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents