Siasa

DC ampinga Lowassa hadharani

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, Kanali Peter Madaha, ameonyesha jeuri ya kumpinga waziwazi Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baada ya kuikataa taarifa ya wilaya hiyo.

na Sitta Tumma, Mwanza


KATIKA hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, Kanali Peter Madaha, ameonyesha jeuri ya kumpinga waziwazi Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baada ya kuikataa taarifa ya wilaya hiyo.


Mkuu huyo wa wilaya alilazimika kumjibu Lowassa hadharani na papo hapo, baada ya kuikataa taarifa hiyo ya wilaya na kisha akamweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa uongozi wake ni dhaifu.


Malumbano hayo yaliyozua gumzo kwa viongozi na watendaji wa serikali yalitokea jana, saa 3:45 asubuhi, Ikulu ndogo jijini hapa wakati mkuu huyo wa wilaya akitoa taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo.


Katika taarifa hiyo, Lowassa alionekana kutoridhishwa nayo hususan katika sekta ya elimu na kilimo, ambayo ilielezwa kuwa na udanganyifu mkubwa hata waziri mkuu kulazimika kuikataa na kusema mkuu huyo wa wilaya hana uongozi thabiti katika wilaya yake.


“Huwezi ukaniambia mimi sina uongozi imara…mimi ni kiongozi na nina miaka 24 nikiwa kama kiongozi wa Serikali ya Tanzania. Mimi ni kiongozi, tena mzuri sana,” alisema DC huyo kwa kujiamini na kwa sauti ya juu.


Katika hali hiyo, Lowassa hakuweza kubishana naye wala kumjibu lolote, isipokuwa alisisitiza kuikataa taarifa hiyo ya wilaya na kuonyesha kusikitishwa na kushangazwa na kauli ya DC huyo.


Mbali na hilo, wakati DC huyo akisoma taarifa hiyo walitoleana maneno makali na Ofisa Kilimo wa Wilaya hiyo, Justus Kulwijila, mbele ya waziri mkuu kwa madai kuwa ofisa huyo wa kilimo alikuwa ametoa taarifa ya uongo kuhusu kilimo cha pamba.


“Waziri Mkuu nikiwa kama mkuu wa wilaya, wilaya yangu hailimi zao la pamba na leo hapa nashangaa umepewa taarifa ya kilimo cha pamba,” alisema mkuu huyo wa wilaya.


DC huyo alikwenda mbali zaidi kwa kumweleza Lowassa kuwa, taarifa ya kilimo cha pamba ndiyo aliyopewa Rais Jakaya Kikwete alipokuwa na ziara ya kikazi mkoani hapa miezi kadhaa iliyopita na kusisitiza kuwa taarifa hiyo ni ya uongo mtupu.


Wakati mkuu wa wilaya akiendelea kumweleza waziri mkuu kuhusiana na suala hilo, ghafla ofisa kilimo huyo alisimama na kukanusha kauli hiyo.


“Mheshimiwa waziri mkuu si kweli kwamba wilaya yetu hailimi pamba…..pamba inalimwa sana na ndiyo maana nimetoa taarifa hiyo ya kilimo,” alisema Kulwijila.


Kutokana na mvutano huo, waziri mkuu alieleza kusikitishwa kwake na utendaji mbovu wa wilaya hiyo ya Nyamagana, na kwamba serikali haitaendelea kuona viongozi wabovu na wasiofaa katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents