Michezo

Azam FC yashtuka yamkataa mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya Yanga SC Jumamosi

Uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, hapo jana umeandika barua rasmi kwenda Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) inayoelezea kutokuwa na imani na mwamuzi Israel Nkongo.

Mwamuzi, Israel Nkongo

Mwamuzi huyo ndiye amepangwa kuchezesha mchezo ujao wa Azam FC dhidi ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex hapo kesho siku ya  Jumamosi majira ya saa 10.00 jioni.

“Kama klabu, itakumbukwa kuwa mechi zetu ambazo mwamuzi huyu (Nkongo) amekuwa akizichezesha zimekuwa na malalamiko mengi na utata mwingi juu ya maamuzi ya uwanjani,” ilisema moja ya nukuu kwenye barua hiyo.

Barua hiyo ilizidi kueleza kuwa moja ya sababu nyingine ya kumlalamikia mwamuzi huyo na kukosa imani naye, ni kitendo chake cha kuzua utata mkubwa kwenye mchezo aliochezesha Mkoani Mbeya wiki moja iliyopita kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City kutokana na uamuzi wake.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyeandika barua hiyo na kutuma nakala kwa Kamati ya Waamuzi, TFF na Yanga, ameweka wazi kuwa kwa kuzingatia uzito wa mchezo huo wameiomba bodi hiyo kubadilisha mwamuzi kwa kumpanga mwingine.

Aidha katika barua hiyo, Mohamed ameongeza kuwa kutokana na timu zote mbili kutoka katika Mkoa wa Dar es Salaam, ameiomba bodi hiyo kumpanga mwamuzi ambaye atatoka nje ya Mkoa huo.

Mbali na Nkongo kupangwa kuchezesha mchezo huo, waamuzi wengine waliopangwa kushirikiana naye ni Josephat Bulali atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba moja, msaidizi namba mbili atakuwa Soud Lila, mwamuzi wa akiba ni Elly Sasii huku Omar Abdulkadir akiwa Kamishna wa mchezo huo, wote wakitoka Dar es Salaam.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents